Thursday, 3 December 2015

MATATIZO YA UZAZI HUUMIZA VICHWA VYA WANANDOA, LEO FAHAMU SABABU ZA MIMBA KUTUNGA NJE YA MFUKO WA UZAZI

Mimba kutungwa nje ya mfuko wa uzazi ni tatizo ambalo huweza kumpata mwanamke yeyote katika maisha yake.

Kwa kawaida mimba hutungwa ndani ya mfuko wa kizazi isipokuwa mara chache huweza kutokea nje ya eneo hilo maalum.

Katika nyumba ya uzazi huwa kuna mirija iitwayo 'Fallopian tube' ambayo kazi yake ni kusafirisha maayai kutoka katika kiwanda chake cha uzalishaji,' ovary' hadi kwenye mfuko wa uzazi. Hapo ndipo mimba hutakiwa kutokea.

Inapotokea hitilafu fulani mimba huweza ikatungishwa kwenye moja ya mirija miwili ya kizazi yaani inaweza kuwa upande wa kulia au kushoto na inapotokea hivyo basi ndio itafahamika kuwa mimba hiyo imetungwa nje ya kizazi.

Inaelezwa kuwa asilimia 95 ya mimba zinazotungwa nje ya 'uterasi' ama nyumba ya uzazi hutokea kwenye mrija hiyo ya 'Fallopian.'

Pale mimba inapotungwa kwenye fallopian husababisha misuli inayozunguka mirija hiyo kushindwa kufanya kazi kutokana na mgandamizo wa mimba inavyokuwa na hivyo kupelekea mishipa inayopita karibu na fallopian kupasuka na damu kutoka kwa wingi jambo ambalo lisiposhughulikiwa kwa haraka huchangia madhara zaidi na hata kupelekea kifo.

Hata hivyo, chanzo cha tatizo hili bado hakijajulikana, ingawaje kuna vihatarishi ambavyo humfanya mwanamke kuwa katika mazingira ya kukubwa na shida hii.

Mambo yanayoweza kumuweka mwanamke kupata tatizo hili ni pamoja na magonjwa ya maambukizi katika mfumo wa uzazi hususani yale yanayosababisha uvimbe.

Sababu nyingine ni pamoja na matumizi ya vitanzi vya kuzuia mimba au kuoteana kwa tishu za kwenye nyumba ya uzazi. Ingawaje si lazima sana vitanzi hivyo kuwa sababu kw akila mwanamke mwenye tatizo hili.

Mbali na sababu hizo, mambo mengine yanayoweza kusababisha mimba kutungwa nje ya nyumba ya uzazi ni uvutaji wa sigara, au upasuaji wa tumbo uliofanyika zamani unaohusu mirija ya fallopian na kusababisha mrija husika kusinyaa.

Magonjwa ya ngono nayo pia ni sababu ya tatizo hili, mfano wa magonjwa hayo ni kaswende au yale yanayosababisha ngozi ndani ya uzazi na mirija ya fallopian kuwa na umbo lisilo la kawaida na kuvimba.

Kwa leo naomba tuishie hapo msomaji wangu, lakini nikusihi endelee kufuatilia tovuti hii kila siku na utapata muendelezo wa mada hii ambapo tutakuja kuangalia dalili zinazoweza kuonekana kwa mwanamke mwenye tatizo hili.

Unaweza kuwasiliana na Tabibu Abdallaha Mandai kwa ushauri zaidi mpigie kwa simu namba 0716 300 200, 0784 300 300, 0769 400 800 au barua pepe dkmandaitz@gmail.com

No comments:

Post a Comment