Friday, 4 December 2015

UJENZI WA BARABARA MWENGE - MOROCCO KUKAMILIKA BAADA YA MIEZI 6

Barabara ya Morocco hadi Mwenge ikiwa katika maboresho.
Ujenzi wa barabara ya Bagamoyo kuanzia Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam, chenye urefu wa kilometa 4.3, kinatarajia kukamilika ujenzi wake ndani ya miezi sita.

Ujenzi wa barabara hiyo ulianza juzi, ikiwa ni siku moja baada ya Rais John Magufuli kuamuru fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe za Uhuru, zikajenge barabara ya Bagamoyo kipande cha Mwenge-Morocco.

Taarifa iliyotolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia Mtendaji Mkuu wake, Patrick Mfugale, ilisema mkandarasi ameshaanza kazi na anatarajia kuikamilisha ndani ya miezi sita.

“Ujenzi umeanza na utakamilika katika kipindi cha miezi sita,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo huku akiomba wananchi wanaofanya shughuli zao kando ya barabara hiyo kupisha ili mradi usikwame.

“Ili utekelezaji usikwame, tunaomba wananchi wanaofanya biashara kandokando ya barabara hiyo, waondoke mara moja, aidha wanaoegesha magari katika eneo la mradi kipindi hiki cha upanuzi waache mara moja,” ilieleza taarifa hiyo ya Mfugale.

Aidha, Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imewataka watembea kwa miguu na wananchi, kutoa ushirikiano katika kipindi hiki cha upanuzi wa barabara hiyo ili kufanikisha ujenzi ndani ya muda uliopangwa.

No comments:

Post a Comment