Friday, 11 December 2015

UKWELI KUHUSU KUPANDA KWA SUKARI WAKATI WA UJAUZITO


Matatzi ya kisukari tumekuwa tukiyazungumza sana kupitia tovuti yetu hii na mara kadhaa tumeshazungumza kuhusu dalili zake chanzo na namna ya kukabiliana na tatizo hili.

Lakini leo ni vyema tuangazie sukari wakati wa Ujauzito (Gestational Diabetes) hii ni aina ya ugonjwa wa kisukari inayowapata kinamama wajawazito.

Mara nyingi aina hii ya kisukari kwa mama mjamzito, hutokea kwa sababu ya mwili kushindwa kutengeneza 'Insulin' ya kutosha kuweza kukidhi mahitaji ya mwili.

Hata hivyo, mara nyingi, aina hii ya kisukari huweza kutoweka mara tu baada ya mama mjamzito kujifungua.

Kufuatia hali hiyo ni vyema ikafahamika kuwa mwanamke anapokuwa katika hali ya ujauzto huweza kuwa katika hatari ya kupatwa na kisukari katika kipindi cha ujauzito na kwamba ugonjwa huo unaweza kumtokea katika hatua yoyote ya ujauzito wake, ingawa mara nyingi hutokea kuanzia nusu ya pili ya ujauzito wake, kwa maana ya kuanzia miezi minne ya mimba.

Wajawazito wenye kisukari huwa katika hatari ya kujifungua mtoto mkubwa, kitu ambacho huweza kupelekea mama kupata ugumu wakati wa kujifungua na hata kupelekea kufanyiwa upasuaji. 

Mtoto kuwa na mwili mkubwa inatoka na kupokea kiwango kikubwa cha sukari kupitia kondo la nyuma la uzazi pindi awapo tumboni sambamba na mama kuwa na hali hiyo ya ugonjwa
wa kisukari.

Kwa kawaida, mtoto anapokuwa tumboni, kongosho la mtoto huhisi uwepo wa kiwango kikubwa cha sukari, kabla ya kongosho hilo la mtoto kuzidisha Insulini kwa wingi katika harakati za kujaribu kutumia sukari ya ziada iliyopo.

Aidha, kina mama wenye tatizo la kisukari wanakuwa katika hatari ya watoto wao kuzaliwa kabla ya wakati au kukumbwa na kifo punde tu baada ya kuzaliwa.

Watoto wanaozaliwa katika hali hiyo, wanaweza kufariki dunia ikiwa sukari itashuka kwa kasi, hivyo kinachotakiwa kufanywa na wataalamu wa afya, ni kumwongezea glukosi ya kutosha punde mtoto anapozaliwa ili kuweza kulinganisha na glukosi ile aliyokuwa akiipata mtoto wakati akiwa tumboni mwa mama.

Miongoni mwa dalili za ugonjwa wa kisukari kwa mama mjamzito ni kupatwa na kiu ya maji ya mara kwa mara, kujisikia uchovu wa mwili wakati wote, kuongezeka uzito wa ghafla isivyo ya kawaida, ikiwa ni pamoja na kukumbwa na unene.

Kwa kawaida, kuanzia siku ya kwanza ya kupata ujauzito hadi siku ya mwisho ya kulea mimba, kwa maana ya miezi tisa, mwanamke anapaswa kuongezeka uzito wa kilo usiozidi 12.5. Kama itatokea uzito huo ukazidi hapo, basi anakuwa katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa wa kisukari.

Dalili nyingine ya kuwa na kisukari kwa mama mjamzito ni kuwahi kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa unaoanzia kilo 2.5 hadi kilo 4.0.

Pamoja na hayo kudhibiti na kufuatilia kwa ukaribu kiwango cha sukari kwa mama mjamzito, ni hatua ya kwanza inayopendekezwa na wataalamu wa afya katika kutibu kisukari. Kutokana na maendeleo makubwa ya kitabibu kuhusiana na ugonjwa huu.

Kuna vifaa vingi vinavyotumika kwa ajili ya kupima mara kwa mara kiasi cha sukari mwilini, ikiwa ni pamoja na vifaa vidogo zaidi ambavyo mtu anaweza akatembea navyo mfukoni.

Halikadhalika mazoezi ni muhimu ya mwili ni muhimu sana katika kipindi chote cha ujauzito kwani yanaweza kumsaidia mama mjamzito kuondokana na uwezekano wa kukumbwa na tatizo hili hii ni  kwa sababu mazoezi hayo husaidia kupunguza kiwango cha sukari kwa kutumia glukosi kwa ajili ya nguvu ya kufanya mazoezi.

Kwa maelezo zaidi wasiliana nasi kwa simu namba 0716 300 200, 0784 300 300, 0769 400 800 au barua pepe dkmandaitz@gmail.com

No comments:

Post a Comment