Saturday, 5 December 2015

WATUMISHI 36 WAPIGWA 'STOP' TRA

Kamishna wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki (mbele kushoto) ambaye ni mshitakiwa namba moja katika kesi ya kula njama za kufanya udanganyifu na kuisababishia hasara serikali ya mabilioni ya fedha, akiwaongoza washitakiwa wenzake wakitoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana baada ya kusomewa mashitaka. (Picha na Yusuf Badi).
WATUMISHI wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), waliosimamishwa kazi kutokana na upotevu wa mapato makubwa ya umma, wameongezeka kutoka tisa wiki iliyopita na kufikia 36.

Idadi hiyo imetokana na hatua ya Serikali kusimamisha kazi watumishi wengine 27 katika geti namba tano la Bandari ya Dar es Salaam, ambao mbali na adhabu hiyo, pia wamewekwa rumande kwa mahojiano na uchunguzi. Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango, alisema hayo jana katika kikao na waandishi wa habari, wakati akielezea utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kushtukiza mwezi uliopita.

Vigogo 36 Taarifa ya Dk Mpango, ilieleza kuwa watumishi 35 katika ngazi mbalimbali wamesimamishwa kazi, wakiwemo hao 27 waliokamatwa wiki hii katika geti namba tano. Hata hivyo, taarifa hiyo haikumjumuisha Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade, ambaye yeye pamoja na watumishi wengine nane walisimamishwa kazi wiki iliyopita, kabla ya hao 27 wa wiki hii.

Waliosimamishwa kazi wiki iliyopita ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki; Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya; Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande; Hamisi Ali Omari (hakutajwa ni wa idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In- Charge), Eliachi Mrema. Pia wamo maofisa Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni, ambao awali walitakiwa kuhamishwa kutoka Dar es Salaam, kwenda mikoani, kabla ya agizo hilo kubadilishwa na kusimamishwa kazi, huku wakizuiwa kusafiri mpaka uchunguzi dhidi yao utakapokamilika.

Rumande, kortini Kwa hatua hiyo ya kushikiliwa kwa maofisa hao 27 wa geti namba tano, idadi ya watumishi wa TRA wanaoshikiliwa Polisi, imeongezeka na kufikia 32 tangu Waziri Mkuu Majaliwa, alipoibua uozo katika ofisi hiyo. Wengine ni Masamaki (56), Mponezya (45), Mpande (28), Omari (48) na Eliachi (31) ambao jana walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7.

Washitakiwa hao pamoja na wafanyakazi wengine wa Bandari Kavu ya Azam (AICD), walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka mawili ya uhujumu uchumi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi. Mbali na hao watumishi wa TRA, wengine ambao ni wafanyakazi wa Bandari Kavu (ICD) ya Azam ni Mkuu wa Ulinzi na Usalama, Raymond Louis (39) na Meneja Ashraf Khan (59).

Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Timony akisaidiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa, aliwasomea washtakiwa mashtaka ya kula njama za kufanya udanganyifu na kuisababishia Serikali hasara ya fedha hizo. Alidai katika tarehe tofauti kati ya Juni Mosi na Novemba 17 mwaka huu sehemu isiyofahamika, washtakiwa hao walikula njama za kuidanganya Serikali kuhusu Sh bilioni 12.7, kwa madai kuwa makontena 329 yaliyokuwa kwenye Bandari Kavu ya Azam (AICD), yametolewa baada ya kodi zote kufanyika, jambo ambalo si kweli.

Katika mashtaka mengine, inadaiwa kati ya siku hizo, kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao vizuri, washtakiwa waliisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 12.7. Hakimu Shahidi alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo washtakiwa hawaruhusiwi kujibu mashitaka yanayowakabili. Dhamana Hata hivyo, upande wa utetezi ulidai mshtakiwa Eliachi ana mtoto wa miezi tisa na bado ananyonya, hivyo aliomba Mahakama itoe maelekezo.

Upelelezi wa kesi hiyo bado hakujakamilika na Hakimu Shahidi aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 17, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena. Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washtakiwa hao walipelekwa katika gereza la Keko na Eliachi alipelekwa gereza la Segerea. Uchunguzi, panga pangua Katika hatua nyingine, Dk Mpango ameagiza watumishi wote wa mamlaka hiyo, kuwasilisha taarifa sahihi ya orodha ya mali zote wanazomiliki kwa ajili ya uhakiki wa kina.

Amesema watumishi hao, wanatakiwa kuwasilisha taarifa hizo kwa uongozi wa juu wa mamlaka hiyo ifikapo Desemba 15 mwaka huu. Kwa mujibu wa Dk Mpango, mtumishi yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo vyovyote vya ubadhirifu, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi kulingana na makosa atakayokutwa nayo.

“Vile vile mamlaka hii inaendelea kupanga upya safu ya watumishi wake ili kudhibiti upotevu wa mapato ya kodi na kuondoa mianya ya uvujaji,” alisema Dk Mpango. Aliwataka watumishi waadilifu wa TRA, kuendelea kuchapa kazi bila hofu na kuongeza kuwa Serikali inatambua mchango wao kwa maendeleo ya Taifa, lakini kwa wale wasio waadilifu Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya dola, itaendelea kuwabaini na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Alisema mamlaka inachukua hatua za kiutawala na kikanuni ili kuondoa upungufu wote, unaotoa mwanya kwa bandari kavu kuondoa makontena bila kufuata taratibu za forodha, ikiwa ni pamoja na kuwaondosha kwenye utumishi wa umma wafanyakazi wasio waadilifu. Dk Mpango alisema wataongeza idadi ya wafanyakazi kwenye bandari kavu, ili kuwa na udhibiti wa uondoshaji shehena kwa saa 24.

Chanzo: Habari Leo

No comments:

Post a Comment