Thursday, 19 May 2016

Leo ni zamu ya kufahamu umuhimu wa mbegu za boga kiafya


MABOGA hutokana na tunda liitwalo boga. Tunda hilo asili yake haijafahamika vizuri ingawaje baadhi ya tafiti zinasema asili yake ni Amerika Kaskazini.

Zao la maboga mara nyingi hushamiri zaidi katika msimu wa joto na inashauriwa kupanda zao hili mwanzoni mwa mwezi Julai hasa katika udongo unaotunza maji vizuri.

Hata hivyo, zao hilo huweza kuathirika iwapo  kutakuwa na upungufu wa maji au joto, lakini pia linaweza kuathirika linapopandwa katika udongo usiochuja maji vizuri.

Maboga ni moja ya chakula bora na muhimu kwa siha ya mwili wa mwanadamu endapo yataandaliwa vizuri.

Mbegu za maboga zina kiwango kingi cha protini na vitamin. Inaaminika kuwa mbegu hizo zinaweza kupunguza mafuta kwenye mishipa ya damu na kwamba gramu moja ya mbegu za maboga huwa na protini sawa na glasi moja ya maziwa.

Watu wengi wanaweza kudharau mbegu za maboga pengine kwa kutokufahamu faida zake, lakini ukweli ni kwamba ni miongoni mwa mbegu zenye faida kubwa mwilini, kwani huweza kuzuia na kutibu hata baadhi ya magonjwa hatari yaliyoshindikana hospitalini.

Mbegu za maboga zina kiwango kingi cha madini aina ya magnesium, ambayo ni muhimu kwa afya ya moyo na uimarishaji wa mifupa pamoja na mishipa ya damu, huku ikiongeza ufanisi wa utumbo mpana

Aidha, mbegu hizo zina kiwango cha madini aina ya 'zinc', ambayo faida yake mwilini ni uimarishaji wa kinga za mwili, hali kadhalika zinc huimarisha nguvu za kiume.

Kutokana na kuwa na kiwango kingi cha 'zinc', tafiti zinaonesha kuwa mafuta ya mbegu zenyewe za maboga huweza kutumika kama dawa ya kutibu saratani ya kibofu.

Mbali na hayo, mbegu hizo zina virutubisho vinavyotoa kinga dhidi ya magonjwa ya ini na moyo.

Halikadhalika mbegu za maboga zina virutubisho vingi vyenye uwezo wa kuzuia magonjwa yote ya uvimbe mwilini, ikiwa ni pamoja na kuvimba miguu, vidole na hata majipu.

Mbegu za maboga pia ni chanzo kizuri cha kamba lishe, kutokana na sifa hiyo boga linaweza kuwekwa kwenye orodha ya vyakula ambavyo husaidia kuondoa tatizo la ukosefu wa choo au kupata choo kigumu.

Matumizi ya boga pia husaidia kuongeza unyevunyevu kwenye ngozi na hivyo kuwasaidia wale wenye matatizo ya ngozi kavu hii ni kutokana na boga kuwa na vitamin E ya kutosha pamoja na kirutubisho kiitwacho 'antioxidant'.

Maboga pia yana vitamin 'A' yakutosha ambayo husaidia kulinda ngozi dhidi ya kuharibika na kuunda seli mpya ndani ya ngozi. Pia ndani ya boga kuna vitamin C ambayo nayo huhitajika sana katika kuhakikisha afya ya ngozi inakaa vizuri zaidi siku zote.

Kwa maelezo zaidi au ushauri unaweza kuwasiliana na Tabibu Mandai kwa simu namba 0716 300 200, 0784 300 300, 0769 400 800 au barua pepe dkmandaitz@gmail.com 

No comments:

Post a Comment