Wednesday, 20 July 2016

Anza leo kutumia karafuu upate faida hizi za kiafya

KARAFUU ni kiungo ambacho kimekuwa kikitumika mara kwa mara hususan katika mapishi.

Kiungo hiki mti wake huwa na shina lilinyooka na hukua kufikia kimo cha mita 10 hadi 12, lakini pia ni moja ya kiungo ambacho kimekuwa kikitumika sana nchini India na China ili  kuwasaidia kulinda kuoza meno na kuondoa tatizo la harufu mbaya kinywani.

Hapa nchini kiungo hicho hupatikana zaidi katika visiwa vya Pemba na Unguja. Karafuu inaelezwa kuwa ni kiungo kilicholetwa na sultani mmoja visiwani humo. Jambo jema ni kwamba Zanzibar sasa inashika namba za juu duniani katika kuzalisha kwa wingi zao hilo.

Wataalam wanasema katika karafuu kuna virutubisho vingi vinavyohitajika katika mwili wa binadamu. Miongoni mwa virutubisho vinavyopatikana ndani ya karafuu ni pamoja na protini, nyuzinyuzi,  wanga na madini ya chuma 'calcium', 'phosphorus,' , sodium.

Virutubisho vinginine ni pamoja na 'potassium', riboflavin, vitamin B2, vitamin B pamoja na vitamin A na C.

Kiungo hiki kina sifa ya kutuliza maumivu ya meno, kutoa gesi tumboni na kurekebisha mfumo wa umeng'enyaji chakula tumboni kutokana na kuwa na kiwango cha nyuzinyuzi.

Aidha, karafuu pia inapotumika vizuri kwa kufuata ushauri wa wataalam wa masuala ya tiba asili husaidia kuimarisha mzunguko wa damu mwilini na hivyo kuchangia kuboresha uwezo wa kushiriki tendo la ndoa.

Karafuu pia huweza kutumika kama njia ya kufifisha hali ya kichefuchefu na hivyo kumfanya mhusika kutotapika. Hivyo, kiungo hiki kinaweza kuwa msaada kwa kinamama wajawazito ambao baadhi yao huzongwa na hali ya kichefuchefu na hata kutapika wakati wa kipindi cha mwanzo cha ujauzito.

Mbali na karafuu kutumika kama kiungo, pia mafuta ya zao hilo yanaweza kutumika kutuliza maumivu mbalimbali ndani ya mwili wa mwanadamu ikiwa ni pamoja na maumivu ya kichwa, unachopaswa kufanya katika hilo ni kutafuta mafuta hayo pamoja na pamba kisha chovya kwenye mafuta halafu weka sehemu ya mbele ya kichwa cha mhusika (mwenye maumivu ya kichwa). Subiri baada ya dakika 15 utaanza kuona matokeo.

Kiungo hicho pia hutumika katika viwanda kutengenezea dawa za meno kutokana na uwezo wake wa kutunza meno na afya ya kinywa kwa ujumla.

Kwa mujibu wa utafiti uliowahi kuchapishwa mwaka 2011 katika Jarida la Asia Plant Science and Research inaelezwa kuwa karafuu husadia kutibu vidonda vya mdomo na kuimarisha afya ya fizi pamoja na kuzuia meno kuoza.

Pamoja na hayo, mafuta ya karafuu yanaelezwa kuwa na vinasaba vya 'eugnol' ambavyo vimekuwa vikitumiwa na madaktari wa meno kuondoa matatizo ya meno na fizi.

Sanjari na hilo, karafuu pia hutumika katika masuala ya urembo hususan mafuta yake katika kusugulia mwili yaani 'scrub'.Hivyo, karafuu na mafuta ya karafuu ni mazuri kwa ajili ya kutunza ngozi hasa kwa ngozi yenye mba na mabaranga kwani huifanya ngozi kuwa nzuri.

Mbali na hayo pia karafuu hutengenezewa sabuni ambazo ni nzuri kwa kuondoa maradhi ya ngozi kama vile harara, vipele na chunusi na kuifanya iwe nyororo na yenye kuvutia. Siyo hayo tu lakini pia karafuu hutumika kutengenezea mafuta mazuri kwa sababu ina harufuu ya kipekee inayovutia.

Hayo ni machache kuhusu faida za karafuu, kama utakuwa na swali au maoni unaweza kuwasiliana nami kwa simu namba +255 716 300 200, +255 784 300 300, +255 769 400 800 au barua pepe dkmandaitz@gmail.com

1 comment: