Sunday, 1 January 2017

Mambo matano muhimu yatakayorahisisha maisha yako mwaka 2017

Inawezekana kuna mambo mengi uliyapanga kuyafanya mwaka 2016 lakini huenda ulishindwa kuyatimiza yote.

Sasa leo ni Januari 1, 2017 nimeona tuambizane haya machache ambayo huenda yatakusaidia kufanikiwa kutimiza malengo yako mwaka huu 2017.


Kwanza lazima uwe na malengo ya kiafya
Hili ni muhimu kwa sababu malengo yoyote hutimia endapo utakuwa na afya njema, lakini unapokuwa na magonjwa mara kwa mara itakuwa ngumu kwako kutimiza mipango yako.Hivyo kwa mwaka huu 2017 jitahidi kufanya uchunguzi wa afya yako mara kwa mara, lakini pia hakikisha unajilinda na kuthamini na kutambua umuhimu wa afya yako kuwa bora.

Mwaka huu 2017 jiulize ni aina gani ya afya unayoihitaji? Unataka uwe namna gani kiafya mwaka huu kutoka sasa Januari? 

2: Weka malengo ya kifamilia
Anza kujiuliza unahitaji uishi wapi? Unahitaji kuoa au kuolewa na nani? Unahitaji uwe na watoto wangapi? Unahitaji familia yako iwe kwenye mfumo upi? nakadhalika. Tambua kuwa ni muhimu sana ufahamu ni nini unachokitaka juu ya maisha yako binafsi na familia yako. Hebu jifunze kuweka malengo kwa ajili ya familia yako na kuyafatilia mara kwa mara na hata kama  huna familia muda huu au mwaka huu ila weka malengo yatakayokuongoza kujua ni familia ya namna gani unayoitaka

3. Tenga ,malengo ya kifedha

Jiulize ni kiasi gani cha fedha unachotaka umiliki kuanzia mwaka huu? Kumbuka kuwa usipojua fedha unazotaka kumiliki huwezi kupata fedha hizo kwa sababu hata ukipata fedha nyingi utaona nyingi na utashindwa kufanyia chochote kwa sababu haukuweka malengo ya kuzitumia.

4. Malengo ya Kitabia.

Jiulize ni tabia gani uliyonayo inayokufanya usipige hatua mbele na kufikia mafanikio makubwa unayoyahitaji? Je, wewe ni mtu wa kulala sana? Je, unapenda sana kushinda vijiweni na kusema watu wengine? Je, unapenda sana kuangalia tamthilia, movie au TV, kuchati kwenye simu na mitandao ya kijamii kuliko kusoma vitabu? Je, wewe ni mtu wa kusafiri hata safari zisizo na maana zinazokupotezea fedha? Je, wewe ni mvivu sana wa kujituma hata katika majukumu yako uliyonayo? Je, una hasira au wivu mbaya kwa wengine? Kwa tabia hizo chache na nyingine ambazo sijazitaja hapa ni kama unazo ni vizuri uangalie namna ya kuziacha mara moja ili ufanikiwe katika mambo yako mwaka huu.

5.Malengo ya Kimungu
Malengo haya ni muhimu sana kwako kuliko malengo mengine yoyote yale katika maisha yako. Watu wengi sana ni wepesi wa kujiwekea malengo ya kifedha, mapato, mahusiano, biashara, uwekezaji, nakadhalika; lakini si watu wa kukumbuka kuweka malengo ya kiroho ambayo ndio muhimu zaidi kwa ajili ya maisha yao yote yaani hapa duniani na baada ya duniani. Hivyo ni vyema ukatambua kuwa unahitaji kuwa na malengo kwa ajili ya maisha yako ya badae baada ya kuondoka duniani.

Kwa maelezo na ushauri wasiliana nasi kwa simu namba 0716 300 200/ 0784 300 30/ 0769 400 800 au barua pepe dkmandaitz@gmail.com

No comments:

Post a Comment