Thursday, 29 June 2017

Mchanganyiko wa matunda unaoimarisha kinga za mwili


Waswahili walisema ‘kinga ni bora kuliko tiba’ licha ya kwamba wengi wetu kwa sasa tumekuwa tuki puuza usemi huo wa wahenga.

Hii inajidhihirisha pale ambapo serikali kupitia wizara yake ya afya inapotangaza kampeni za chanjo mbalimbali za magonjwa muamko huwa ni hafifu sana na wengi wakisubiri waumwe kwanza au waone dalili ndipo waende hospitali jambo ambalo ni hatari zaidi kwa afya.

Kwa kawaida binadamu tuna kinga ndani ya miili yetu ambazo majukumu yake ni kuhakikisha mwili muda wote upo salama na haushambuliwi na magonjwa mbalimbali, lakini uimara wa kinga hizo za mwili hutegemea sana na mtindo mzima wa maisha ya mhusika kuanzi vyakula anavyokula na kunywa pamoja mazingira kwa ujumla wake.

Mbali na vyakula, lakini pia mwili huweza kujiimarisha zaidi kupitia njia mbalimbali yakiwemo mazoezi.

Pamoja na hayo ni vyema ikafahamika kuwa kwa kawaidia mwili wa binadamu huwa na uwezo wa kujitibu wenyewe bila kuhitaji dawa ya aina yoyote kutokana na uumbaji wa Mwenyezi Mungu, lakini jambo hilo hutegemea sana na namna nzima ya maisha ya mhusika kuanzia ulaji , unywaji na mazingira yote yanayomzunguka kwa ujumla wake.

Kwa mujibu wa Mtaalam wa masuala ya lishe bora kutoka kampuni ya Mandai Products, Abdallah Mandai anaeleza kuwa, vipo vyakula, viungo, matunda na mbogamboga ambavyo vikiandaliwa vizuri huweza kusaidia kuimarisha kinga za mwili na kumfanya mhusika kutozongwa na magonjwa ya mara kwa mara.

Mandai anasema, miongoni mwa vitu vyenye nafasi ya kuongeza uimara wa kinga za mwili ni pamoja na asali, kutokana na kimiminika hicho kuwa na kiwango kikubwa cha virutubisho na madini ambayo kwa pamoja husaidia kujenga na kuimarisha kinga za mwili. Unachopaswa kufanya ni kulamba kijiko kimoja cha chakula chenye asali kila siku kutwa mara tatu.

Aidha, mbali na asali mtaalam huyo anabainisha kuwa ulaji wa matunda mara kwa mara nayo ni njia nzuri ya kujenga na kuimarisha kinga za mwili kutokana na matunda mengi kuwa na vitamin mbalimbali ikiwemo vitamin C ambayo moja ya kazi yake kuu ni kuimarisha kinga hizo.

Mbali na vitamini hizo, pia ndani ya matunda kuna madini mbalimbali ambayo nayo husaidia kulinda afya ya meno na mifupa kwa ujumla na hivyo kumfanya mhusika kuwa na afya njema zaidi.


Aidha, matumizi ya juisi ya karoti nayo husaidia kuimarisha kinga za mwili na kumlinda mhusika dhidi ya magonjwa mbalimbali yakiwemo matatizo ya macho, hii ni kutokana na karoti kuwa na vitamin A ya kutosha.

Pamoja na hayo, mtaalam huyo amesema, juisi hiyo ya karoti inasifika kwa kuimarisha mifupa, kutokana na kuwa na madini ya ‘potassium’ ambayo hupatikana ndani yake.

Sambamba na hayo, Mandai ameeleza namna mchanganyiko wa matunda ya aina tatu yaani matikitimaji, tufaa (apple) pamoja na karoti ambavyo huweza kujenga na kuimarisha kinga za mwili endapo yataandaliwa vizuri.

Matunda hayo kwa pamoja yatahitajika kuandaliwa vizuri kwa kuyaosha na kutoa maganda pamoja na mbegu na kisha kuchanganywa kwa pamoja na baadaye kusagwa, huku ukianza na tufaa na matikitimaji na baadaye kuchanganywa kwa pamoja na karoti iliyosagwa .

Baada ya mchanganyiko huo kusagika unashauriwa kuchuja mara moja na kuweka kwenye jagi na baadaye kuongeza kiwango kidogo sana cha sukari au kutoweka kabisa, kisha utatumia mchanganyiko huo kunywa asubuhi na jioni kila siku kikombe kimoja .

Fanya zoezi hilo angalau kwa miezi miwili mfululizo na itakusaidia sana katika kukukinga dhidi ya magonjwa ya mara kwa mara.

Makala hii pia unaweza kuipata kwenye gazeti la Tanzania Daima la Juni 29/ 2017

Unaweza kuuliza maswali mbalimbali kwa kupiga simu namba 0716 300 200/ 0784 300 300/ 0769 400 800 au barua pepe dkmandaitz@gmail.com

Pia unaweza kupakua App yetu kwa kuingia kwenye playstore kisha tafuta mandai products na utaidownload kisha utakuwa unapata kila taarifa zetu kupitia simu yako kila siku.

No comments:

Post a Comment