Tuesday, 20 February 2018

Akwilina kuzikwa Ijumaa Rombo

                                         Marehemu Akwilina Akwilini
MWILI wa Akwilina Akwilini aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam, unatarajiwa kuagwa katika viwanja vya chuo hicho Alhamisi (kesho kutwa) na kisha kusafirishwa siku hiyo hadi Rombo mkoani Kilimanjaro ambako anatarajiwa kuzikwa Ijumaa.

Akwilina alifariki siku ya Ijumaa iliyopita Dar es Salaam baada ya kupigwa risasi alipokuwa ndani ya daladala.
Mmoja wa wanafamilia ya marehemu, Festo Kavishe amesema ripoti ya upasuaji imeonesha kuwa Akwilina alifariki dunia baada ya shambulio la risasi katika kichwa chake ambalo liliingia kichwani kupitia upande wa kushoto na kutokea wa kulia ambalo lilimjeruhi vibaya..
Kavishe amesema familia imetosheka na ripoti hiyo iliyotolewa na hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambako kulifanyika uchunguzi huo na hivyo kuandaa taratibu za mazishi hayo. Alisema familia ilitaka kufahamu picha kamili ya vile alivyouawa Akwilina.
Wakati huo huo maofisa wa Polisi jijini Dar es Salaam wamewataka viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwenda mbele yao kuhojiwa kutokana na kifo hicho.
Taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na masuala ya kigeni, John Mrema amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar esbsalaam jana Jumatatu lilitoa amri kwa viongozi saba wa Chadema kuripoti katika ofisi hizo ili kuhojiwa.
Miongoni mwa viongozi  waliotakiwa kwenda katika ofisi hizo ni pamoja na mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, katibu mkuu wa chama hicho, Dk. Vicenti Mashinji na naibu katibu mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, John Mnyika.
Akwiline alifariki baada ya kupigwa risasi kimakosa wakati wa maandamano ya wafuasi wa chama hicho yaliotibuliwa na maafisa wa polisi siku ya Ijumaa iliyopita.
Taarifa za zilizotolewa awali na jeshi hilo linasema maafisa wa polisi walikuwa wakijaribu kuwatawanya waandamanaji kwa kile walichokitaja kuwa maandamano haramu yaliofanywa na Chadema wakati ambapo risasi hiyo ilipita katika kioo cha nyuma cha daladala na kumpiga kichwani Akwilina aliyekuwa ndani ya gari hilo.

No comments:

Post a Comment