Monday, 19 February 2018

Akwilina kuzikwa Rombo


Marehemu Akwilina Akwilini
MWILI wa marehemu Akwilina Akwilini aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam unatarajiwa kusafirishwa hadi Rombo, mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
Wazazi wa marehemu walipata taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo Ijumaa baada kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa ni polisi baada ya makabiliano kati yao na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Ndugu wa marehemu Damiani Swai amesema watachukua hatua baada ya matokeo ya uchunguzi kutoka Jeshi la Polisi ambalo linaendelea nao sasa.
Mwanafamilia huyo amesema Akwilini alikuwa na ndoto za kufika mbali kielimu lakini zimezimwa akiwa katika harakati za kuzifikia.
Serikali kupitia Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako imesema itagharamia mazishi ya mwanafunzi huyo.
Hadi wakati huu taarifa zilizo ni kwamba polisi sita wanaendelea kuhojiwa kutokana na kifo cha mwanafunzi huyo.
Kumekuwa na shinikizo kutoka vyama vya upinzani kikiwemo ACT Wazalendo, vijana na Shirika la wanafunzi nchini kumtaka waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba kujiuzuru nafasi hiyo baada ya kisa hicho cha kusikitisha.


No comments:

Post a Comment