Wednesday, 21 February 2018

Asilimia 96 ya kaya nchini zinatumia kuni, mkaa


              Msitu ulioharibiwa kwa ajili ya kuni na mkaa

Suleiman Kasei

ASILIMIA 96 ya kaya hapa nchini zinatumia nishati ya mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia huku asilimia nyingine 91 za kaya katika mkoa wa Dar es Salaam zikihusika na matumizi hayo.

Meneja Mradi wa Mkaa Endelevu (TTCS), Charles Leonard amebainisha hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari wanaoshiriki mafunzo kuhusu usimamizi shirikishi wa misitu na mkaa endelevu yaliyoandaliwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) yanayofanyika wilayani Kilosa mkoani Morogoro.

Leonard amesema pamoja na kuwepo elimu dhidi ya madhara ya kutumia mkaa na kuni, bado hali si nzuri hasa katika maeneo ambayo hayajafikiwa na mradi.

Amesema ukataji mkaa na kuni unachangia upoteaji wa mapato ya sh. bilioni 220 pamoja na hekta 500,000 kuharibiwa kwa mwaka.

"Asilimia 99 ya kaya hapa nchini zinatumia mkaa na kuni na Dar es Salaam pekee pamoja na kuwepo kwa umeme asilimia 91 ya wakazi wake wanatumia mkaa hali ambayo ni hatari sana," amesema.

Meneja huyo amefafanua kuwa kwa mwaka uvunaji wa mkaa unafikia tani 2.3, hivyo kama hakutakuwa na jitihada za haraka uharibifu wa mazingira utakuwa mkubwa zaidi.
Amesema takwimu zinaonesha kuwa nchi inaingiaza sh. trilioni 2.2 kwa mwaka ila madhara yanayobakia ni makubwa zaidi hivyo ni jukumu la kila mdau kutoa elimu ya umuhimu wa kutunza mazingira na upandaji miti.

Meneja huyo alisema TTCS katika kusaidia utunzaji wa mazingira imetoa elimu kwa vijiji 30 katika mkoa wa Morogoro.

Amesema vijiji 20 vipo wilaya ya Kilosa, vitano Mvomero na Morogoro vijiji vitano na kuwa mradi huo utaendelea hadi Novemba  mwaka 2019.

Kwa upande wake Ofisa Mawasiliaono wa TFCG, Bettie Luwuge amesema shirika lao limekuwa likitoa elimu kwa wanavijiji kuhusu utunzaji misitu shirikishi ambapo hadi sasa zaidi ya wanavijiji 60,000 katika Ukanda wa Mashariki na Pwani ya Kusini wamepatiwa mafunzo mbalimbali kuhusu umuhimu wa kushiriki utunzaji misitu.

Luvuge amebainisha kuwa katika kuhakikisha elimu wanayotoa inakuwa endelevu wameamua kushirikisha wahariri na waandishi wa habari waandamizi kwa kuwapatia mafunzo ili wawe mabalozi katika eneo hilo.


No comments:

Post a Comment