Tuesday, 20 February 2018

Boko Haram washindwa jaribio la kuwateka wanafunzi wa kike


Wanamgambo wa Boko Haram
WANAFUNZI wa kike na walimu wao kaskazini mashariki mwa Nigeria, wamefanikiwa kukimbia jaribio la shambulio lililofanywa na wanamgambo wa Boko Haram kwenye shule yao.
Walioshuhudia wamesema wanamgambo hao waliokuwa na magari waliwasili kwenye mji wa Dapchi, jimbo la Yobe hapo jana Jumatatu na kuanza kufyatua risasi na kulipua vilipuzi.
Kuliposika sauti hizo wanafunzi na walimu wao walifanikiwa kutoroka. Mwezi Aprili mwaka 2014, Boko Haram waliwateka nyara wasichana 270 wa shule katika mji wa kaskazini mashariki wa Chibok.
Wakazi na raia waliojihami huko Dapchi wanasema wanaamini wanamgambo hao walikuwa na mpango wa kuwateka nyara wasichana.
Baada ya kupata shule ikiwa bila mtu wanamgambo hao waliipora. Wanasema kuwa vikosi vya jeshi la Nigeria vikisaidiwa na ndege za jeshi, baadaye vilizima shambulio hilo.
Mwezi Septemba mwaka uliopita zaidi ya wasichana wa shule 100 wa shule ya Chibok waliunganishwa na familia zao kwenye sherehe katika mji mkuu wa Nigeria Abuja.
Sehemu kubwa ya wasichana hao waliokolewa mwezi Mei kufuatia mpango uliokumbwa na utata wa kubadilishana wafungwa na serikali ambapo makamanda wa Boko Haram waliachiliwa.
Lakini zaidi wa wasichana 100 bado wanashikiliwa na Boko Haram na haijulikani waliko.
Wanamgambo wa Boko Haram wamekuwa wakiendesha harakati za kutaka kuwa na taifa lao la kiislamu kaskazini mwa Nigeria. Mzozo huo unaaminiwa kusababisha vifo vya maelfu ya watu.No comments:

Post a Comment