Thursday, 15 February 2018

Hatimaye Rais Zuma ajiuzulu   Jacob Zuma
RAIS wa Afrika Kusini Jacob Zuma amejiuzulu baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa chama chake.
Kupitia hotuba yake iliyopeperushwa kwa njia ya televisheni, Zuma amesema anajiuzulu mara moja huku akiongeza kuwa hakubaliani na uamuzi wa chama cha ANC.
Chama cha ANC kilikuwa kimemuambia aondoke madarakani au akabiliwe na kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.
Zuma mwenye umri wa miaka 75 amekuwa akikabiliwa na shinikizo za kumtaka ampe nafasi makamu wake Cyril Ramaphosa, ambaye ndiye sasa kiongozi mpya wa chama hicho.
Zuma ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2009, amekumbwa na shutuma nyingi za ufisadi.
Mapema Jumatano, polisi walivamia nyumba ya familia tajiri ya Gupta ambayo Zuma ana uhusiano wa karibu nayo.
Zuma alijiuzulu kwa njia gani?
Alianza hotuba kwa kucheka na kufanya mzaha na waandishi wa habari.
Baada ya kuwashukuru wale ambao amefanya nao kazi kwa miaka kadhaa, alisena ghasia na migawanyiko ndani ya ANC imesabisha ajiuzulu
"Hakuna maisha yatapotea kwa sababu yangu wala ANC haiwezi kugawanyika kwa sababu yangu. Kwa hivyo nimefikia uamuzi wa kujiuzulu kama rais wa nchi mara moja," amesema
"Licha ya kutokubaliana na uamuzi wa chama changu, siku zote nimekuwa mwanachama mwenye nidhamu wa ANC.
"Ninapoondoka, nitaendelea kuwatumikia watu wa Afrika Kusini sawa na ANC, chama ambacho nimekitumikia maisha yangu yote,”amebainisha Zuma.
BBC


No comments:

Post a Comment