Mwanaume akipatiwa huduma ya tohara katika moja ya mikoa hapa nchini ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya kutahiri wanaume ili kuwakinga na hatari ya kuambukizwa magonjwa mbalimbali ukiwemo Ukimwi.
WAKATI hapa nchini kampeni ya tohara kwa wanaume ikitiliwa
mkazo, Iceland ipo katika harakati za kuwa taifa la kwanza barani Ulaya kupiga
marufuku tohara ya wanaume.
Utamaduni huo unaotekelezwa sana na Wayahudi pamoja na Waislamu,
huenda ukazua hisia kali kuhusu uhuru wa kuabudu nchini humo.
Muswada ambao kwa sasa umewasilishwa mbele ya bunge la Iceland,
unapendekeza hadi miaka sita jela kwa mtu yeyote atakayetekeleza tohara hiyo
isipokuwa tu kwa ajili ya sababu za kimatibabu.
Wakosoaji wanasema hatua hiyo ambayo imezua hisia miongoni mwa
viongozi wa kidini barani Ulaya itafanya maisha ya Wayahudi na Waislamu nchini
Iceland kuwa magumu.
Mmoja kati ya wanaume watatu duniani huwa amepashwa tohara
sababu kuu ikiwa ni ya kidini au ile ya kitamaduni.
Wayahudi wengi na Waislamu wanahofia kwamba suala hilo linaweza
kutumiwa kulenga dini hizo mbili wakitaja wasiwasi kama huo kuhusu mavazi ya
kidini mbali na uchinjaji wa wanyama kwa lengo la kutumia nyama yao.
Muswada huo unasema tohara ya wavulana wadogo inakiuka haki yao
ya kibinadamu na ni kinyume na azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya mtoto.
Inaangazia suala hilo sanjari na lile la ukeketaji wa wanawake
ambao tayari umepigwa marufuku katika mataifa kadhaa ya bara la Ulaya.
Muswada huo unasema tohara hiyo inatekelezwa bila kutilia
maanani uchungu unaompata mwathiriwa na kuongezea kuwa hatua hiyo hutekelezwa
katika nyumba ambazo sio safi bila madaktari bali na viongozi wa dini.
''Kuna hatari kubwa ya maambukizi chini ya hali hiyo ambayo
huenda ikasababisha kifo.muswada huo unasema kuwa wazazi wana haki ya kutoa
mwelekeo wa kidini kwa watoto wao, lakini haki hizo haziwezi kuwa juu ya haki
za mtoto'', unasema muswada huo.
Wavulana wanaotaka kufanyiwa tohara kutokana na sababu za kidini
au kitamaduni wanaweza kufanya hivyo watakapofikisha umri ambao wanaelewa ni
nini kinachoendelea wakati wa tohara hiyo.
Taifa la Iceland lina raia 336,000 ikiwemo jamii za Wayahudi na
Waislamu. Linadaiwa kuwa na Wayahudi 250 na Waislamu 1,500.
Chanzo BBC
No comments:
Post a Comment