Thursday, 22 February 2018

Isaidieni serikali kujenga miundombinu ya maji

 Ujenzi wa miundombinu imara ya maji ni muhimu kwa kuwa inachochea maendeleo.

WADAU sekta ya maji na usafi wa mazingira nchini, wametakiwa kuisaidia serikali kutekeleza vipaumbele vyake ambavyo ni ujenzi wa miundombinu ya maji, utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vyake.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk.Dicson Nzunda, ametoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano mkuu  wa wadau wa uwajibikaji katika sekta ya maji na usafi wa mazingira (WASH) mjini Dodoma.

Mkutano huo umeandaliwa na Mtandao wa maji na usafi wa mazingira (Tawasanet), ambapo wadau hao wanajadiliana changamoto zilizopo katika sekta ya maji na usafi wa mazingira pamoja na kubadilishana uzoefu.

Dk. Nzunda amesema ni muhimu wakati wote wadau kuisaidia serikali kutekeleza majukumu yake badala ya kuja na vipaumbele vyao visivyoendana na malengo ya serikali.

Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya maji, utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji pamoja na usafi wa mazingira.

“Usafi ni sehemu ya utu, uhai na afya ya mwanadamu anayeishi maisha bora. Hivyo, kazi hii ni vema ikawa endelevu ili kuendeleza heshima na utu wa watu wetu,” amesema.

Aidha, Dk. Nzundu ameongeza kuwa serikali imeweka nguvu kubwa katika kuimarisha ushiriki wa raia kwenye utawala bora ikiwemo kuelimisha na kubadilishana taarifa mbalimbali.

“Kimsingi wizara yangu inabeba jukumu kubwa katika kusimamia na kuimarisha ubora  wa huduma na mawasiliano mazuri  baina ya taasisi za serikali,”amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa maji na usafi wa mazingira(Tawasanet), Herbet Kashililah, amesema mkutano huo utawasaidia kujua changamoto ambazo zipo katika sekta ya maji na usafi wa mazingira.No comments:

Post a Comment