Saturday, 10 February 2018

Jafo awapa kibarua Tarura  waziri wa Tamisemi Selemen Jafo


Joyce Kasiki,Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, ameagiza Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), kuelekeza bajeti yao ya mwaka 2018/2019 kujenga barabara ya kilomita  tatu kutoka kata ya Chang’ombe hadi Chuo cha Mipango.

Ujenzi huo unalenga kutatua kero ya barabara kwa wakazi wa eneo hilo mjini hapa.

Jafo ametoa maagizo hayo alipokua anazindua soko jipya la Chang’ombe lililojengwa na Serikali kwa kusaidiana na wafanyabiashara pamoja na Mbunge wa Dodoma mjini, Anthon Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri wa
Kazi, Ajira na Vijana.

Soko hilo ambalo lilianza kujengwa mwaka 2017 na kukamilika mwaka huu, lina wafanyabiashara wapatao 342 wanauza bidhaa mbalimbali.

Hata hivyo, soko hilo bado linachangamoto mbalimbali kama kukosekana mifereji ya kutiririsha maji taka, vumbi na barabara za  lami ili kurahisisha ushushaji wa mizigo sokoni hapo.

Waziri Jafo amesema serikali inawekeza miundombinu ya hali ya juu katika Mkoa wa Dodoma ikiwemo mtandao wa barabara za lami katika maeneo mbalimbali pamoja na taa za barabarani na ujenzi wa dampo la kisasa.

“Kwa kuwa serikari inahamia Dodoma, hivyo basi
miundombinu mbalimbali lazima iendelee kujengwa na kurekebishwa,” amesisitiza Jafo.

Aliwapongeza wananchi kwa kushirikiana na halmashauri ya manispaa ya Dodoma kukamilisha ujenzi wa soko la kisasa hali akiwapongeza na kusema “soko hili limejengwa kwa gharama nafuu sio kama masoko mengine yanayojengwa kwa gharama kubwa mno”.

Ameupongeza uongozi wa mkoa wa Dodoma pamoja na mkuu wa mkoa huo, Dk. Binilith Mahenge na Mbunge wa Dodoma mjini Anthony Mavundekwa jitihada zao za kuleta maendeleo mkoani hapo.


No comments:

Post a Comment