Wednesday, 21 February 2018

Kipindupindu chaua 20 Dodoma

Mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk. James Charles akizungumza katika moja ya mikutano  mkoani humo.

UGONJWA wa kipindupindu mkoani Dodoma, umeua watu 20 miongoni mwa 471 waliougua ugonjwa huo katika kipindi cha miezi minne.

Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk.James Charles amethibitisha hilo jana wakati akizungumza na wanahabari mjini hapa huku wilaya ya Mpwawa ikiongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi zaidi.

“Kuanzia Oktoba mwaka jana mkoa ulipopata mlipuko wa ugonjwa huu, ulioanzia wilaya ya Chamwino katika kijiji cha Mlowa na baadaye kusambaa katika baadhi ya wilaya za mkoa wetu, watu 20 wamepoteza maisha yao hadi jana (juzi), Februari 19," amesema Dk.Charles

Amefafanua kuwa ugonjwa  huo ulidhibitiwa baada ya kuingia hapo Oktoba mwaka jana, lakini ilipofiki Desemba mwaka huo, mlipuko ukaongezeka  kwa kasi katika wilaya za Mpwapwa na Chamwino.

"Tangu kulipuka kwa ugonjwa huu, hadi kufikia jana (juzi)   jumla ya watu 471 waliugua, miongoni mwao 20 wamefariki," amesema.

Kwa mujibu wa Dk. Charles, wilaya ya Mpwapwa ndiyo  imetoa wagonjwa wengi zaidi ambapo miongoni mwa 471,  wagonjwa 322 wametoka katika wilaya hiyo.

Amesema Mpwawa imekuwa na wagonjwa wengi zaidi kwa kuwa inakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba mkubwa wa maji ukizingatia kipindi cha mlipuko ndicho watu wanakwenda katika shughuli za kilimo ambako wanatumia maji yoyote wanayoyapa.

Pia ameitaja changamoto nyingine inayochochea tatizo hilo ni uchafu wa mazingira, ulaji wa vyakula usiozingatia kanuni za usafi na maandalizi ya vyakula yasiyo salama katika maeneo ya biashara.

Ili kukabiliana na ugonjwa huo, Dk.Charles  amesema mkoa kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, umeongeza udhibiti lakini pia unatoa  elimu ya afya kwa wananchi ili kuutokomeza.

Hata hivyo, amesema wagonjwa walikuwa katika makambi mbalimbali wanapatiwa matibabu wamepungua na hadi jana walikuwa wamebakia 13 tu.

No comments:

Post a Comment