Friday, 23 February 2018

Magufuli, Kenyatta waagiza kumalizwa tofauti baina ya Kenya na Tanzania

         Rais Dk. John Magufuli wa Tanzania (kushoto), Uhuru Kenyatta wa Kenya

RAIS Dk. John Magufuli na Uhuru Kenyatta wa Kenya wamekutana mjini Kampala, Uganda na kuahidi kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili.

Wamewaagiza mawaziri wao kutatua tofauti ndogondogo zinazojitokeza katika biashara kati miongoni mwao.
Marais hao wametoa maagizo hayo walipokutana hoteli ya Munyonyo mjini Kampala muda mfupi kabla ya kuanza vikao vya mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki.
Uhusiano kati ya Tanzania na Kenya ulikuwa unaonekana kudorora wiki za karibuni hasa kutokana na hatua ya Tanzania kuwakamata na kuwateketeza vifaranga kutoka Kenya na pia kuwapiga mnada ng'ombe wa watu wa jamii ya Wamaasai kutoka nchini humo.
Wamesema wanataka kuona biashara baina ya nchi hizo inazidi kuimarika na bidhaa zinauzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo bila vikwazo.
"Yapo mambo madogomadogo yanajitokeza katika biashara kati ya Kenya na Tanzania, tunataka kwa haya yote mawaziri wa Kenya na wa Tanzania mkae myatatue.
“Sisi hatuna tatizo, mambo mengine madogomadogo mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana, mnatakiwa myatatue ninyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawasawa" amesema Dk. Magufuli, tamko ambalo limeungwa mkono na Kenyatta.
Wametoa maagizo hayo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi upande wa Tanzania na Kenya ni Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Monica Juma na Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Ushoroba wa Kaskazini wa Kenya Peter Munya.

No comments:

Post a Comment