Tuesday, 27 February 2018

Mahakama ya Rufaa kanda ya Dodoma kusikiliza rufani 28

Mary  Meshack, Dodoma

MAHAKAMA ya Rufani ya Tanzania imeanza vikao vyake katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, mkoani hapa vitakavyodumu hadi Machi 16, mwaka huu.

Kiongozi wa jopo la majaji hao, Mbarouk Salim Mbarouk amesema majaji wanne watasikiliza na kutoa hukumu kwa kesi 28 zinazohusu jinai, madai na maombi ya madai.

Jopo la majaji wanne linaloundwa na Jaji Richard Mziray, Jaji Rehema Mkuye na Jaji Jacobs Mwambengere likiongozwa na Jaji Mbarouk Salim Mbarouk limeanza kusikiliza kesi nne za rufaa, tatu zikiwa za jinai na moja ya maombi ya madai.

Akizungumzia tuhuma za rushwa katika taasisi za umma ikiwemo mhimili huo wa sheria, Jaji Mbarouk amesema katika ngazi hiyo ya mahakama ya rufaa suala hilo halipo.

Jaji Mbarouk amewaomba wananchi kufika katika mahakama hiyo ili kujifunza mienendo ya kesi na taratibu mbalimbali ili kuondokana na mitazamo tofauti kuhusu mahakama.

Wiki tatu tangu kuanza kwa mwaka mpya wa kimahakama, mahakama kuu Kanda ya Dodoma inakuwa mwenyeji wa vikao vya mahakama ya Rufaa ambavyo ni vya juu zaidi vya utoaji haki hapa nchini.

No comments:

Post a Comment