Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto)
akipatiwa taarifa ya hali ya hewa kwa usafiri wa anga na Meneja wa Utabiri wa
Hali ya Hewa, Samwel Mbuya wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wakati
alipotembelea makao makuu ya mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Suleiman Kasei
NAIBU Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye ameitaka Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA), kujitangaza umuhimu wake katika nyanja ya kiuchumi na
kijamii kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Mhandisi Nditiye ametoa
agizo hilo alipotembelea makao makuu ya TMA ambapo alizungumza na bodi ya mamlaka
hiyo, menejimenti na wafanyakazi kwa lengo la kutambua majukumu yao na
kufuatilia utekelezaji wake ili kufikia malengo ya serikali ya kuwatumikia
wananchi.
Akizungumza na Bodi,
menejimenti na wafanyakazi, Mhandisi Nditiye amewaeleza kuwa TMA ni chombo
muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa na wananchi kwa ujumla kwa
kuwa sekta ya usafiri wa anga, majini, ujenzi wa majengo mbalimbali,
miundombinu ya barabara na reli, afya, kilimo na mazingira vyote vinategemea
taarifa za hali ya hewa kutoka kwenye mamlaka hiyo.
“Mtambue kuwa hakuna ndege
inayoweza kutua wala kuruka bila kupata taarifa kutoka kwenu, vile vile
mkandarasi anayejenga reli ya kisasa ya SGR naye anategemea taarifa zenu kwa
kiasi kikubwa, hivyo mtambue ninyi ni muhimu na mjitangaze,” amesema Mhandisi
Nditiye.
Mwenyekiti wa Bodi ya
TMA, Dk. Buruhani Nyenzi wakati akiwasilisha taarifa yake kwa Mhandisi Nditiye amesema
mamlaka hiyo ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya taifa na wananchi kwa kuwa inatoa
taarifa na huduma za hali ya hewa nchini ambayo imewezesha uokoaji wa maisha ya
watu na mali zao.
Naye Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa TMA, Dk. Hamza Kabelwa amemueleza Mhandisi Nditiye kuwa wahitaji wa
taarifa za hali ya hewa kutoka kwa taasisi na wadau mbalimbali kwa ajili ya
kutekeleza shughuli za kiuchumi na kijamii wamekuwa wengi na teknolojia ya
utabiri wa hali ya hewa na utoaji wa taarifa zake umebadilika.
No comments:
Post a Comment