Monday, 19 February 2018

Mhandisi Nditiye: Toeni nafasi ya mafunzo kwa vitendo

Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) akimtunuku cheti kwa kufaulu vizuri masomo yake mmoja wa wahitimu Shekha Habibu Humudi wakati wa mahafali ya 16 ya Chuo cha Bandari Dar es Salaam yaliyofanyika chuoni hapo jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia wa kwanza kulia ni Mkuu wa Chuo hicho Dk. Joseph Kakeneno na wa kwanza kushoto ni mjumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania mzee Renatus Mkinga.


NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye ameielekeza Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), pamoja na menejimenti ya mamlaka hiyo, kutoa nafasi kwa wanachuo wa Chuo cha Bandari Dar es Salaam kufanya mafunzo kwa vitendo wakati wa masomo yao kwenye bandari zote nchini.

Mhandisi Nditiye ameyasema hayo akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 16 ya Chuo cha Bandari Dar es Salaam ambapo wahitimu 521 wametunukiwa cheti cha kuhitimu mafunzo yao katika ngazi ya astashahada na stashahada ya mafunzo ya aina mbalimbali ikiwemo usimamizi wa shughuli za meli na bandari.

Amesema nia ya Serikali ni kufikia malengo ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli ya kuboresha bandari zote, kuongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi wa sekta ya usafirishaji majini ili kukuza uchumi wa taifa.

Wakati akisoma hotuba yake kwa wahitimu hao, Mhandisi Nditiye amewataka kutumia vyeti vyao na taaluma waliyoipata kukitangaza vema Chuo cha Bandari Dar es Salaam ndani na nje ya nchi.

Amesisitiza kuwa wanaoajiriwa kuwa wafanyakazi wa bandari mbalimbali wawe wamehitimu chuo na kuwa na elimu inayotakiwa. Vile vile amemwagiza Mkuu wa Chuo cha Bandari Dk. Joseph Kakeneno kujenga zahanati kwa ajili ya kutoa huduma za tiba kwa wanachuo na jamii ya Chuo hicho.

Naye mjumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamzi wa Bandari Tanzania Renatus Mkinga ambaye amemwakilisha Mwenyekiti wa bodi wa Mamlaka hiyo, Prof. Ignas Rubalatuka amewataka wanachuo kusoma kwa bidii ili waweze kuajiriwa na kufanya kazi mahali popote iwe ndani au nje ya nchi.

Aidha, wahitimu wa chuo hicho wamemshukuru Dk. Kakeneno kwa kufanikisha upatikanaji wa ithibati sita za kozi mbalimbali kati ya nane zinazohitajika na kumwomba mgeni rasmi Mhandisi Nditiye kumsaidia Dk. Kakeneno kupata ithibati nyingine mbili zilizosalia.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Nditiye ametoa mwezi mmoja kwa Chuo cha Bandari Dar es Salaam kwa kushirikiana na wataalamu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kurudisha majengo ya chuo hicho, uwanja wa michezo na mali zote zilizokuwa zinatumiwa na Chuo cha Hoteli na Utalii ambazo ziko ndani  ya eneo la Chuo cha Bandari ya Dar es Salaam yarudishwe kwenye Chuo cha Bandari.


No comments:

Post a Comment