Friday, 16 February 2018

Mjane wa Aboud Rogo ahukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka kumi



MAHAKAMA moja nchini Kenya imemhukumu mwamamke Haniya Said Saggar kifungo cha miaka kumi kwa kosa la kupanga njama ya kufanya shambulio la kigaidi.

Mahakama imempata na hatia ya kuratibu shambulio la bomu la petroli lililotekelezwa dhidi ya kituo cha polisi jijini Mombasa miaka miwili iliyopita.
Haniya ni mjane wa Aboud Rogo, ambaye aliaminika kuandaa shughuli za kundi la wanamgambo wa Al Shabaab nchini Kenya.
Kwenye hukumu yake, hakimu alisema kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwamba Haniya aliwasiliana na mmoja wa wanawake watatu waliolitekeleza shambulio hilo.
Mwanamke huyo, Tasnim Yakub, alikuwa amesilimu kutoka Ukristo miezi mitatu kabla ya shambulio, ikiwa ndio muda pia ambao alipata kujuana na Haniya.
Mahakama imefahamishwa pia kwamba wawili hao waliendelea kuwasiliana hadi muda mfupi kabla ya shambulio hilo.
Inadhaniwa pia kwamba Tasnim aliwavutia wanawake wawili aliojiunga nao kukiteketeza moto kituo cha polisi na hata kujaribu kumdunga kisu askari. Wote watatu walipigwa risasi na kuuawa.
Ripoti ya ushahidi uliotokana na uchunguzi umebaini kwamba kipakatilishi cha Tasnim kilikuwa na fasihi zenye itikadi kali baadhi ambazo zilichapishwa na kiongozi wa kidini mweye misimamo mikali Aboud Rogo - marehemu mumewe mshtakiwa.
Sheikh Rogo aliunga mkono wazi wazi kundi la Al Shabaab na pia alitetea mauaji ya wakristo.
Rogo mwenyewe aliuawa kwa kupigwa risasi mara kumi na sita na watu wasiojulikana mwaka 2012, tukio ambalo lilizua maandamano na tafrani jijini Mombasa.
Rogo aliaminika kuwa na uhusiano wa karibu na raia wa Uingereza Samantha Lethwaite, al Maarufu 'white widow', anayetuhumiwa kufadhili mauaji nchini Kenya, na ambaye bado anasakwa na Polisi wa kimataifa, Interpol.

Haniya Said Saggar (kulia), akizungumza na wakili wake Aboubakar Yusuf kortini. 
BBC

No comments:

Post a Comment