Thursday, 22 February 2018

Mjumita yampa onyo Waziri KigwangalaRevocatus Njau (kushoto), akikabidhi mzinga wa nyuki kwa wajasirimali wa mkoa wa Tanga.

Suleiman Kasei, Kilosa

MWENYEKITI wa Bodi ya Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita), Revocatus Njau amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Hamis Kigwangala kuachana na ndoto ya serikali kuchukua misitu ambayo inatunzwa na wananchi kwani atasababisha nchi kuingia katika jangwa.

Njau ameyasema hayo katika mafunzo ya wanahabari kuhusu usimamizi wa misitu na mazingira yanayofanyika wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.

Amesema hivi karibuni alimsikia waziri huyo akiweka bayana dhamira yake ya kutaka kurejesha misitu inayohifadhiwa na wananchi jambo ambalo halikubaliki.

Mwenyekiti huyo alisema ndoto anayoota waziri huo haina faida kwa nchi kwani wananchi waneonesha uwezo wa kutunza rasilimali misitu kwa ufanisi mkubwa.

"Waziri Kigwangala anaota ndoto ambayo alikuwa anaota Adolf Hitler kuwa atatawala dunia hivyo namshauri aachane na ndoto yake ya kurejesha misitu inayosimamiwa na jamii pamoja na Serikali kuu atasababisha jangwa," amesema.

Njau amesema kwa takribani miaka 30 sasa wananchi wamekuwa wakijitolea kutunza na kulinda misitu ya asili na kijamii kwa ufanisi mkubwa hivyo kitendo cha kuleta mabadiliko kinaweza kuibua matatizo makubwa.

Ameongeza kuwa Mjumita pekee inasimamia misitu yenye ukubwa wa hekta milioni 1.8 katika vijiji 452, wilaya 30 na mikoa 13 hivyo haingii akilini kuona kiongozi tena wa chama tawala CCM anakuwa na mawazo tofauti na ilani yake.

Ofisa Uraghibishi wa Mradi wa Kuleta Mageuzi Katika Sekta ya Mkaa Tanzania kutoka Mjumita, Elida Fundi amesema  dira  yao ni kuona jamii ya Watanzania inayojali, kulinda na kutumia misitu na rasilimali zitokanazo na misitu kiundelevu.

Fundi amesema pia dhima yao ni kuhamasisha, kuwajengea uwezo, kuwaunganisha, kuwaimarisha wadau wote na mitandao ya usimamizi wa misitu ili jamii ijiamini, ishiriki, ishawishi, itoe uamuzi na kutumia  kwa njia endelevu.

Aidha, amesema Mjumita imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kunakuwepo sera ambazo zitakuwa rafiki na sekta ya mkaa.

Ofisa huyo amesema iwapo jamii itapata elimu sahihi kuhusu misitu na dhana nzima ya mkaa endelevu itapewa msukumo rasilimali misitu itakuwa salama.

No comments:

Post a Comment