Mkaa ni nishati muhimu kwa matumizi ya nyumbani, lakini katika maeneo mengi watayarishaji wa nishati hiyo hawazingii utunzaji wa mazingira kwa kuwa wanateketeza miti kwa kiwango kinachotisha.
Suleiman Kasei
MTANDAO wa Jamii
wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) umetoa mapendekezo manne kwa serikali
ili kuhakikisha kuwa upotevu wa misitu nchini unadhibitiwa.
Mapendekezo hayo
yametolewa na Ofisa Uraghibishaji wa Miradi Mjumita, Elida Fundi wakati
akiwasilisha mada kwa wanahabari
mwishoni mwa wiki.
Fundi ametaja
pendekezo la kwanza ni kuandaa sera ambazo zitatambua thamani ya huduma ya
mifumo ikolojia na mazao ya misitu, hasa inayohusu uamuzi na mgawanyo wa ardhi.
Amesema pendekezo
jingine ni kupitia sera ili kuweka uhusiano wa moja kwa moja wa
biashara, misitu na malengo ya kusimamia ardhi yenye misitu.
“Pia sera iunge
mkono miradi inayotokana na misitu (mbao, mkaa) ambayo inanufaisha jamii ili kutoa
motisha kwa usimamizi endelevu wa misitu ya asili; na kufikia mahitaji ya kiuchumi
ya mazao ya misitu,” amesema.
Ofisa huyo
ameongeza kuwa wakati umefika kupitisha kanuni ili mazao ya misitu ambayo
yamevunwa bila kanuni za usimamizi endelevu yasihalalishwe kwenye vituo vya
ukaguzi.
Aidha, Fundi amesema
visababishi vikuu vya upotevu mkubwa wa misitu nchini ni mahitaji makubwa
ya ardhi kwa ajili ya kilimo ambapo taarifa ya Naforma ya mwaka 2015 inasema
takribani hekta 372,816 za misitu zinapotea kila mwaka na wakati huo huo
taarifa ya Serikali ya Takwimu za msingi za Hewa Ukaa ya mwaka 2016 inaonesha kuwa
hekta 469,000 za misitu inapotea kila mwaka.
Ofisa huyo amesema
tafiti za hivi karibuni zinaonesha kuwa kati ya asilimia 70 hadi
80 ya matukio yaliyosababisha upotevu wa misitu nchini ni
ufyekaji wa misitu kwa ajili ya upanuzi wa mashamba (kilimo).
Amesema sera
zilizopo hazijaweza kutoa muongozo wa namna ya kutatua kisababishi
kikuu cha upotevu wa misitu nchini akitolea mfano sera ya misitu haina tamko linalozuia
kubadilisha eneo la misitu kuwa shamba la kilimo, hususan maeneo muhimu ya
kiikolojia kwa kuboresha uratibu na wizara ya kilimo, wizara ya ardhi.
Kwa upande wake Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Kuhifadhi
Misitu Asili Tanzania (TFCG), Bettie Luwuge amesema pamoja na kuwepo sera nzuri
ni jukumu la serikali kutenga kutengeneza
maeneo madogo ya usimamizi wa mkaa ndani ya misitu katika hifadhi za vijiji kwa
ajili ya uzalishaji wa mkaa endelevu.
Amesema TFCG, Mjumita na Shirika la Kuendeleza Nishati Tanzania
(TaTEDO) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswiss
(SDC) wamedhamiria kupigania utunzaji wa misitu na mazingira kupitia
Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS ), hivyo Serikali
inapaswa kuunga mkono jitihada hizo.
No comments:
Post a Comment