Saturday, 24 February 2018

Mkikita kuanzisha shamba kubwa la mipapai

Mkurugenzi wa Mkikita, Adam Ngamange (kulia), akizungumza na wafanyabiashara Visentini Steffano kutoka Italia na Duncan Washington wa Kenya wakati wa mazungumzo yanalenga kununua mashine za kisasa za kutengenezea jusi ya papai, embe na nanasi.

Suleiman Kasei, Dar es Salaam 

MTANDAO wa Kijani Kibichi Tanzania (Mkikita), upo katika hatua za mwisho za kuanzisha shamba lenye ukubwa wa hekari 300 kwa ajili ya kilimo cha mipapai wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mkikita, Adam Ngamange wakati akizungumza na dkmandai baada ya ufunguzi wa mafunzo ya wanachama zaidi ya 300 wa taasisi hiyo leo Dar es Salaam.

Mkurugenzi huyo amesema wamelazimika kuanzisha kilimo katika eneo kubwa ili waweze kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ambalo limeanza kukua kwa kasi kubwa.

Amesema katika kipindi cha siku za hivi karibuni kumekuwepo na hitaji kubwa la papai hivyo wanatarajia kupitia wanachama 300 walioshiriki mafunzo hayo kutumia nafasi hiyo kuwekeza katika shamba hilo lilopo Bagamoyo.

Ngamange amesema kwa muda mrefu Mkikita imekuwa ikifanya kazi na mkulima mmoja mmoja hivyo kwa sasa wanataka kubadilisha mfumo kwa kuwaweka wakulima pamoja hasa wanapohitaji kufanya kilimo cha aina moja.

“Tupo katika hatua za mwisho kuanziasha kilimo cha papai katika shamba kumbwa huko Bagamoyo ambapo matarajio yetu ni shamba hilo kuwa chini ya wanachama wa Mkikita ila pia wanaruhusiwa kukodisha,” amesema.

Ngamange amefafanua kuwa kuanzia Machi Mosi mwaka huu shamba hilo litaanza kufanyiwa matayarisho ili upandaji uanze ifikapo Septemba ili mwakani waanze kuvuna zao hilo na kuuzwa nje ya nchi.

Amesema wamefanya mazungumzo na wafanyabiashara wa maduka makubwa nchini Uturuki ambapo wameonesha nia ya kuhitaji papai kutoka Tanzania hivyo soko ni la uhakikika na kwamba mazungumzo hayo yatamalizika mwezi Mei ambapo wao wataenda nchini humo.

Mtendaji huyo amesema kupitia ziara hiyo watajifunza kuhusu teknolojia ya uzalishaji kuanzia maaandalizi ya shamba na pembejeo ambazo zinapaswa kutumika katika kilomo husika.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa dhamira yao Mkikita ni kuona wakulima wa papai, nanasi, embe na mbogamboga wananufaika na kilimo kama ilivyo nchi nyingine duniani.

Amebainisha kuwa kwa sasa Mkikita ina wanachama zaidi ya 12,000 huku matarajio yao ni kuwa na wanachama milioni 1 ifikapo 2020 ili waweze kupanua soko la bidhaa mbalimbali.

Ngamange amesema kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya mtazamo kwa baadhi ya wakulima ambao bado wanafikiria mfumo wa mkulima kulima, kupakia na kutafuta soko ambao haupo kwa sasa.

“Bado wapo wakulima ambao wanafikira za kizamani wanataka walime, wavune wapakie na kupeleka sokoni mfumo huo hauhitajiki kwa sasa kwani tupo sisi tutatafuta soko,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Greenbase Agro Input, Charles John ambaye pia ni mtaalam wa kilimo amewataka wanakulima walioshiriki mafunzo hayo kuzingatia kanuni za kilimo bora ili waweze kupata mavuno mengi.

Amesema kilimo cha papai kinalipa iwapo mkulima atafuata kanuni za kilimo pamoja na kutumia mtandao wa Mkikita kama kiungo cha soko la ndani na nje.

”Kilimo siku zote ili kiwe na tija ni lazima uzingatie kanuni na taratibu ukilazimisha huwezi kunufaika, lakini yote kwa yote kwa ulimwengu wa sasa mtandao unahitajika ili uweze kuuza mazao yako popote duniani na Mkikita ndiyo jibu sahihi,” amebainisha.

John amesema ili kufanikiwa katika kilimo cha papai nilazima kuwepo mbegu bora, maji ya kutosha, mbolea, udongo wenye rutuba, teknolojia, mafunzo na  pembejeo nyingine.

Ametaja sifa ya mbegu bora ya papai ni pamoja na kuzaa kwa wingi, kuhimili magonjwa, matunda kudumu bila kuharibika na rangi nzuri ambayo inakubalika sokoni.No comments:

Post a Comment