Monday, 19 February 2018

MSCL kudhibiti mapato ya kieletroniki

Mwandishi Wetu


 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akikata tiketi ya kieletroniki mara baada ya kuzindua mfumo wa tiketi hizo katika Meli ya MV Clarias, mkoani Mwanza.
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameitaka Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), kuhakikisha inafunga kamera katika maeneo mbalimbali ya ukaguzi ili kudhibiti vitendo vya hujuma katika mifumo ya kampuni hiyo hususan kwenye mapato. 

Ametoa rai hiyo jijini Mwanza mara baada ya kuzindua mfumo mpya wa ukatishaji tiketi kwa njia ya kielektroniki katika Meli ya MV Clarias na kusisitiza kuwa matumizi ya mfumo huo mpya yaende sanjari na elimu stahiki kwa watumishi wanaoutumia mfumo huo katika kukatisha tiketi. 

“Niwapongeze sana kwa hatua hii ya kuingia kwenye mfumo wa kielektroniki katika utoaji huduma lakini niwatake sasa kuongeza kamera kwenye maeneo yote unapofanyika ukaguzi ili kudhibiti mianya yote inayoweza kujitokeza ya kuhujumu mapato ya kampuni,”amesema Prof. Mbarawa. 

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza kwenye shirika hilo ili kupata faida itakayowezesha kujitegemea na kuagiza kuwa kwa sasa kila fedha inayopatikana itumike vizuri sababu shirika limeanza kupata faida. 

Aidha, Prof. Mbarawa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Serikali Mtandao (eGA), kutengeneza mfumo kama huo kwa ajili ya Shirika la Reli Nchini (TRL), ili kudhibiti uvujaji wa mapato. 

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Serikali Mtandao, Dkt. Jabir Kuwe, amesema mfumo huo umetengenezwa na wakala ili kuiwezesha taasisi hiyo kudhibiti mapato kwani utarahisisha huduma kwani abiria ataweza kukata tiketi akiwa sehemu yoyote nchini. 

Naye Kaimu Meneja Mkuu wa MSCL, Erick Hamis, amesema mfumo wa kielektroniki umeanza kwa meli moja ya MV Clarias inayofanya Safari zake kutoka Mwanza kuelekea kisiwa cha Ukerewe ambapo katika mpango wa baadaye kampuni inategemea kutumia mfumo huo kwenye meli zake zote. 

Ameongeza kuwa kampuni imejiwekea mpango wa miaka miwili wa kukarabati meli Tisa za kampuni hiyo ambapo hadi sasa meli Tatu zimeshakarabatiwa na kuanza kazi wakati hatua ya kuanza ukarabati kwa meli zilizobaki uko katika hatua nzuri

Mfumo huo mpya wa kielektroniki wa ukatishaji tiketi katika kampuni hiyo umegharimu sh. milioni 50.

No comments:

Post a Comment