Thursday, 22 February 2018

Mwanamume atolewa uvimbe wa karibu kilo mbili kwenye ubongo


                  Santlal Pal akiwa na mkewe baada ya kutolewa uvimbe

MADAKTARI nchini India wamefanya upasuaji wa kipekee na kuondoa uvimbe wa uzani wa kilo 1.8 kutoka kwa mwanamume Santlal Pal mwenye umri wa miaka 31.
Madaktari hao wanasema huo huenda ukawa uvimbe mkubwa zaidi kuwahi kutolewa kwenye ubongo wa binadamu.
Upasuaji huo, ambao ulidumu kwa muda wa saa saba, ulifanyika 14 Februari 14 katika hospitali ya Nair mjini Mumbai magharibi mwa nchi hiyo.
Lakini taarifa za upasuaji huo hazikutangazwa moja kwa moja kwa sababu madaktari hawakuwa na uhakika iwapo ulifanikiwa.
"Sasa ni suala tu lake kupona, lakini maisha yake hayamo hatarini tena," Dk. Trimurti Nadkarni, mkuu wa upasuaji wa mfumo wa neva, amesema.
Santlal Pal, mwuzaji duka kutoka jimbo la Uttar Pradesh kaskazini mwa India, amekuwa akiishi na uvimbe huo kwa miaka mitatu.
Madaktari wanasema Pal alipoteza uwezo wake wa kuona kutokana na uvimbe huo.
Hata hivyo, kuna matumaini kwamba huenda akapata uwezo wa kuona tena baada ya kupona.
Mke wake ameliambia gazeti moja nchini India kwamba alikuwa ameambiwa na madaktari katika hospitali tatu tofauti Uttar Pradesh kwamba uvimbe huo hauwezi kuondolewa.
"Visa kama hivyo huwa hatari sana," Dk. Nadkarni amesema, na kuongeza kwamba Pal alihitaji painti 11 za damu wakati wa upasuaji huo.
Aidha, alitumia mtambo wa kumsaidia kupumua kwa siku kadha baada ya upasuaji huo.No comments:

Post a Comment