Tuesday, 27 February 2018

Naibu waziri abaini ukosefu wa mawasiliano Ziwa Nyasa, Tanganyika

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (kushoto) akisalimiana na Meneja wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) mkoa wa Rukwa Peter Kuguru alipowasili wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na uchukuzi mkoani humo.


Suleiman Kasei

NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amefanya ziara ya kikazi kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwa wananchi waishio kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa na Tanganyika katika maeneo ya vijiji mbalimbali viliyopo kwenye mkoa wa Njombe, Mbeya na Rukwa.

Mhandisi Nditiye amefanya ziara hiyo ili kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi waishio kwenye mwambao huo ili kujiridhisha kuhusu uwepo wa huduma hizo ambapo Serikali kupitia Wizara hiyo inaipatia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ruzuku inayoziwezesha kampuni za simu za mkononi kufikisha huduma za mawasiliano vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.

Katika ziara hiyo, Mhandisi Nditiye amebaini uwepo wa mawasiliano hafifu kwenye baadhi ya maeneo na mahali pengine hamna mawasiliano yoyote kwa wananchi waishio mwambao wa Ziwa Nyasa na Tanganyika.

“Nimesafiri kwa boti ndani ya Ziwa Nyasa kutoka eneo la Lupingu, Ludewa mkoani Njombe hadi Matema mkoani Mbeya na sasa kwenye bandari hii ya Kabwe mkoani Rukwa, nimeshuhudia mwenyewe ukosefu wa mawasiliano ya uhakika kwa wananchi waishio kwenye mwambao wa ziwa ambapo lolote likitokea ukiwa ndani ya ziwa huwezi kabisa kuwasiliana,” amesema.

Amebainisha kuwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa wananchi kuwasiliana kwa kuwa mawasiliano yanachangia ukuaji wa pato la wananchi na taifa kwa ujumla, pia yanawezesha na kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo husika.

Amesema kuwa tayari Wizara kupitia UCSAF imefanya tathmini ya kufikisha huduma za mawasiliano kwa kuzipatia ruzuku kampuni za simu za mkononi ili ziweze kujenga minara ya simu za mkononi.

No comments:

Post a Comment