Monday, 19 February 2018

Nyama tani moja kuteketezwa

Suleiman Kasei


Nyama inapokwisha muda wake wa matumizi huharibiwa

ZAIDI ya kilo 1000 za nyama iliyoisha muda wa matumizi mali ya Kampuni ya Frostan Limited ya Dar es Salaam, inatarajiwa kuteketezwa kwa moto na Kampuni ya Safety Weste Incinerator ya Mkuranga mkoani Pwani.
Nyama hiyo inachomwa baada ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kuibani kuwa imeisha muda wa matumizi na kuiandikia barua Kampuni ya Frostan Limited kutoendelea kuuza na kuagizwa kuichoma kwa mujibu wa sheria.
Awali nyama hiyo ilikuwa ichomwe siku ya Ijumaa Februari 16 wilayani Kibaha lakini Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilizuia uchomaji wa nyama hiyo kutokana na eneo husika kukosa sifa za uchomaji.
Akizungumzia shughuli hiyo Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kinondoni, Mohamed Msangi amesema baada ya uchomaji kushindikana siku ya Ijumaa unafanyika leo huko Mkuranga.
Msangi amesema NEMC ilifanya ukaguzi katika eneo la Kibaha ambalo lilipendekezwa na kubainika kuwa halikuwa na sifa ya kufanya kazi hiyo ikiwa ni pamoja na kampuni husika kukosa usajili kwa kazi hiyo.
Kwa mujibu wa barua ya TFDA, inaweka bayana kuwa kampuni hiyo inapaswa kuteketeza nyama hiyo kwa wakati kutokana na kukiuka taratibu za nchi na kimataifa kuhusu ubora wa vyakula.
Barua hiyo imebainisha kuwa utaratibu wa kubadilisha muda wa matumizi ya chakula au nyama yoyote iliyoisha muda wake haupo  kwa mujibu wa sheria.
Barua hiyo ilibainisha kuwa,  vyakula vinazingatia kuwepo kwa muda fulani na kwamba kitendo cha muda husika wa chakula kuongezwa huku muda umeisha ni hatari na ni sumu.
Wiki iliyopita Ofisa Afya na Mratibu wa TFDA, Manispaa ya Kinondoni, Fabian Nahonga alisema aliyekuwa anasubiriwa ni mwenye nyama hiyo kuonesha eneo la uchomaji kama walivyomuagiza.
Nahonga amesema walikagua na kubaini uwepo wa nyama hiyo ambapo waliwekea alama ili isitumike tena.
Amesema, baada ya ukaguzi wao ilibainika kuwa katoni 52 ndizo zinapaswa ambapo baada ya kupima zilipatikana kilo 1,103.52 ambazo ni zaidi ya kilo 1000.
Ofisa afya huyo amesema, dampo la Pugu ambalo lipo Ilala Dar es Salaam haliwezi kuteketeza nyama hiyo jambo ambalo limesababisha kumtaka atafute mahali pa kuchomea.
Nahonga amesema TFDA Kinondoni imepewa jukumu la kusimamia ukaguzi na uteketezaji wa nyama hiyo kutokana na kampuni kuwa katika manispaa hiyo.
Nahonga amesema pamoja na kampuni hiyo kulipia gharama za uteketezaji pia inapaswa kulipia gharama za usimamizi ambapo kama kazi ikifanyika  katika eneo la Dar es Salaam wasimamizi wanalipwa nusu ya posho ya siku na kama itafanyika nje ni posho ya siku nzima.
Alhamisi ya wiki iliyopita Mkurugenzi Mtendaji wa Frostan Ltd, Jean-Francois Pinck, alisema hatua zote muhimu zimekamilika na kwamba matarajio yake ni nyama kuchomwa Ijumaa.

No comments:

Post a Comment