Monday, 19 February 2018

Prof. Mbarawa awataka wananchi Simiyu kulinda miundombinu ya barabara


Mwandishi Wetu

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Mwigumbi-Maswa yenye urefu wa KM 50.3 ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98, mkoani Simiyu. Ujenzi huo umefadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 na umegharimu sh. bilioni 61.46.


WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewataka wakazi wa wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, kuilinda miundombinu ya barabara iliyokamilika kujengwa ili kupunguza gharama za matengenezo ambayo yanaepukika.

Ametoa rai hiyo wilayani hapa, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mwigumbi-Maswa yenye urefu wa KM 50.3 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.

Amesema barabara hiyo itawaunganisha wananchi wa mikoa ya kanda ya ziwa na kukuza uchumi kupitia mazao mbalimbali yanayolimwa kwenye mikoa hiyo.

"Barabara hii sasa imekamilika ni jukumu la kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzie kuilinda na kuhakikisha inadumu kwa kipindi kilichokadiriwa", amesema Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa barabara hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi watakaotumia usafiri wa reli ya kisasa pindi utakapokamilika kwani watatoka kwenye mikoa ya jirani kupandia kwenye stesheni ya Malyampaka ambayo iko kwenye barabara hiyo.

Aidha, amewapongeza Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani humo kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na wananchi kwa kutoa ushirikiano kwa mkandarasi ili kuharakisha ujenzi wa barabara hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Maswa Dk. Seif Shekalaghe, ameishukuru Serikali kwa kukamilisha sehemu ya barabara hiyo na kumuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa miundombinu hiyo italindwa ili idumu muda mrefu.

"Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuikamilisha barabara hii kwa kiwango cha lami kwani kwa sasa muda na gharama za usafirishaji wa mazao zitapungua", amesema Dkt. Shekalaghe.

Naye Meneja wa TANROADS, mkoa wa Simiyu, Mhandisi Albert Kent, amesema mradi huo hadi sasa umekamilika kwa asilimia 98 na kazi iliyobaki ni kuweka alama za barabarani na ujenzi umezingatia viwango vinavyohitajika.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Mwigumbi-Maswa yenye urefu wa KM 50.3 imejengwa na Mkandarasi wa Kampuni ya CHICO ambapo imegharimu sh. bilioni 61.46 na zote zikiwa zimefadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.
No comments:

Post a Comment