Tuesday, 27 February 2018

Rais Ramaphosa atangaza baraza jipya la mawaziri

 Rais Cyril Ramaphosa
RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ametangaza baraza lake jipya la mawaziri. Waziri wa zamani wa fedha Nhlanhla Nene amerejeshwa tena katika nafasi hiyo.
Nene alifukuzwa kazi katika nafasi hiyo Desemba mwaka 2015 na Rais wa zamani wan chi hiyo, Jacob Zuma na nafasi yake ikachukuliwa na Des van Rooyen.
Palipotokea anguko la thamani ya randi alilazimika kumfukuza Rooyen na kumchagua Pravin Gordhan, siku nne baadaye ambaye pia alimfukuza kazi siku za mbeleni.
Katika baraza la Ramaphosa, Gordhan amerejea kama waziri wa masuala la biashara.
Aliyekuwa mke wake Zuma, Nkosazana Dlamini-Zuma, ameteuliwa kuwa waziri wa ofisi ya rais.
Ramaphosa, ambaye ni mfanya biashara mwenye umri wa miaka 65, katika hotuba yake ya taifa awali mwezi huu, aliahidi kupambana na rushwa na kuboresha uchumi wa nchi hiyo.
Aliingia madarakani baada ya mtangulizi wake kuondoka katika hali tete, akikataa shinikizo kubwa la kutakiwa kujiuzulu.

Utawala wa miaka tisa wa Zuma ulikumbwa na misukosuko ya shutuma za ufisadi wakati nchi ilikuwa ikipambana na madeni ya ndani pamoja na viwango vya juu vya ukosaji ajira.

No comments:

Post a Comment