Monday, 5 February 2018

Rais Zuma njia panda                            Rais Jacob Zuma

SHINIKIZO kubwa la kutakiwa kujiuzulu linaendelea kumkabili rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma baada ya mazungumzo na maofisa mbalimbali wa ngazi za juu katika chama  chake ANC yaliyofanyika jana.

Haijajulikana iwapo mazungumzo hayo yalihusu nini lakini maofisa waandamizi wa chama hicho leo wanatarajiwa kukutana tena katika mkutano mwingine wa dharura.

Kiongozi wa sasa wa ANC, Cyril Ramaphosa aliichukua nafasi hiyo kutoka kwa Zuma baada ya kukabiliwa na tuhuma za rushwa kwa kiwango kikubwa.

Wadadi wa mambo wanasema wakuu wa chama hicho wanajaribu kuondoa mvutano wa kung'ang'ania madaraka ambao unaweza kukigawanya chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo hapo mwakani.

Hata hivyo, upo ushahidi kuwa kuna mchakato wa kumuondoa rais Zuma madarakani kupitia mfumo rasmi au kwa kuidhinisha hoja bungeni.

Hata hivyo, maofisa sita wakuu wa chama hicho tawala waliwasili mmoja baada ya mwingine Jumapili katika makazi ya rais Zuma mjini Pretoria.

Walinyamaza kimya wakati wa mazungumzo yalipomalizika lakini wameitisha mkutano wa kamati kuu ya chama hicho hivi leo.

Julius Malema, kiongozi wa upinzani na aliyekuwa mfuasi wa chama hicho cha ANC katika mtandao wake wa Twitter anasema  rais Zuma amekataa kujiuzulu.

Zuma anatakiwa kubaki madarakani hadi uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika hapo mwakani, lakini chama hicho kimepoteza umaarufu wake katika muhula wa pili wa kiongozi huyo huku kukishuhudiwa pia kudorora kwa uchumi na tuhuma za rushwa.


No comments:

Post a Comment