Monday, 19 February 2018

Serikali kugharamia mazishi ya mwanafunzi

MWANDISHI WETU Marehemu Akwilina Baftaha

SERIKALI imesema itagharamia shughuli zote za mazishi ya Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa Usafirishaji (NIT), Akwilini Baftaha aliyeuawa Februari 16 kwa kupigwa na risasi akiwa katika daladala katika eneo la Mkwajuni wakati Jeshi la Polisi likipambana na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo aliambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Yusuph Masauni.

Amesema Serikali imepata pigo kubwa kwa msiba huo kwani imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kusomesha elimu hivyo kitendo cha kuuawa hakikubaliki popote.

Ndalichako amesema kifo cha Akwilina kimetokea wakati akiwa njiani kupeleka barua kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.

Waziri huyo amesema marehemu Akwilina alikuwa na ndoto inayoishi ila kutokana na tukio hilo la juzi ndoto hiyo imebadilishwa ghafla.

Amebainisha wizara imelazimika kugharamia msiba huo kama sehemu ya mchango wao kwani tukio hilo linawahusu na kuwa ameagiza mamlaka husika kuanza mchakato wa kugharamia.

"Napenda kutumia nafasi hii kutoa pole kwa ndugu, marafiki, familia, wanafunzi, wananchi na jumuiya ya wanachuo kwa msiba huu mkubwa wa mwanafunzi," amesema.

Waziri huyo ametoa ombi kwa mamlaka za kichunguzi kufanya kazi ya uchunguzi ili wahusika waweze kubainika na hatua za kisheria zichukuliwe.

Kwa upande wake Masauni amesema Serikali kupitia vyombo vyake vya uchunguzi inaendelea kuchunguza na pindi uchunguzi ukikamilika taifa litataarifiwa.

Masauni amesema Serikali inatarajia kutoka na majibu ambayo yatafanya matukio kama hayo ya uvunjifu wa amani yanakoma kuanzia sasa.

"Kitendo hiki cha kupoteza maisha, kujeruhiwa wananchi na askari tunataka iwe fundisho kwa mtu yoyote ambaye anasababisha kupoteza maisha au ulemavu wa mtu na hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa yule ambaye atabainika kutekeleza mauji haya zitachukuliwa," amesema.

Ameongeza kuwa tukio hilo limefanywa na ofisa wa jeshi la polisi kwa kwenda na kinyume na utaratibu uliolezwa wazi Sheria ya Makosa ya Jinai pamoja na PGO ya kukabiliana na matukio ya uhalifu au kiongozi wa kisiasa hatua itachukuliwa.
Masauni amesema wapo viongozi wa kisiasa ambao walidiriki kusema uchaguzi huo hautapita hivihivi hivyo wakibainika hatua zitachukuliwa.

Akizungumzia tukio hilo Mbunge wa Singida Mashariki Chadema, Tundu Lissu amesema matukio ya watu kuuawa hasa nyakati za uchaguzi yanaweza kudhibitiwa iwapo itapatikana Katiba mpya.

Amesema utaratibu wa Jeshi la Polisi kwa sasa ni kutekeleza matakwa ya Serikali iliyopo madarakani na chama tawala hivyo ni jukumu la wao kubadilika ikiwemo kubadilisha katiba.

"Huko mbele tuendako agenda yetu kubwa lazima iwe kukabiliana na mambo haya na ili kufanikiwa katika hilo ni kuwepo kwa Katiba mpya," amesema.No comments:

Post a Comment