Monday, 12 February 2018

Tatizo la umeme Dar kubaki historiaWaziri wa Nishati Merldadi Karemani


SERIKALI imesema jiji la Dar es Salaam litakuwa na umeme wa uhakika tofauti na sasa ambapo umekuwa ukikatika mara kwa mara.

Waziri wa Nishati, Merldadi Karemani ametoa kauli hiyo bungeni Ijumaa alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalum, Lucy Mageleli (Chadema).

Katika swali la nyongeza mbunge huyo alitaka kujua ni lini serikali itafunga transifoma kubwa kwa ajili ya kuondokana na tatizo la kukatika  umeme mara kwa mara katika wilaya ya Kigamboni

“Kwa sasa wilaya ya Kigamboni kuna tatizo kubwa la umeme na umeme umekuwa ukikatika mara 15 kwa siku, kutokana na hali hiyo ni lini serikali itafunga transfoma kubwa kama ilivyo ahidi ili kuondokana na adha hiyo?,” alihoji mbunge huyo.

Awali katika swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum, Neema Mgaya (CCM) alitaka kujua ni lini serikali itawasha umeme katika kijiji cha Itengelo kata ya Saja kutokana na transifoma kufungwa lakini haifanyi kazi.

Akijibu swali la nyongeza la Mageleli, Waziri wa Nishati, alisema kuwa ni kweli katika wilaya ya Kigamboni kuna tatizo kubwa la kukatika umeme lakini serikali inashughulikia jambo hilo.

Hata hivyo, amesema serikali inatarajia kujenga kituo kidogo ambacho kitawezesha jiji la Dar es Salaam kuwa na umeme wa uhakika tofauti na ilivyo sasa.

Amesema kutokana na hali hiyo maeneo mbalimbali katika jiji hilo yatakuwa na umeme wa uhakika ikiwa ni pamoja na wilaya ya Kigamboni.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgaru akijibu swali la msingi amesema kijiji cha Itengelo ni kati ya vijiji vilivyonufaika na mradi wa 

Umeme Vijijini (REA), awamu ya pili uliotekelezwa na mkandarasi Kampuni ya M/S Sengerema Engineering Group Ltd ambaye alipewa kazi ya mradi kwa Mkoa wa Njombe.

Aidha, alisema kijiji cha Itengelo kiliwashiwa Umeme Agosti 22 mwaka jana kwa kufungiwa transifoma 2 pamoja na kuwaunganishia wateja 56 waliolipia. Bunge limeahirishwa Ijumaa.

No comments:

Post a Comment