Wednesday, 21 February 2018

Ukosefu nyumba bora za walimu kikwazo cha ufaulu mzuri Dodoma


Mazingira duni wanayoishi walimu yamebainishwa na wadau wa elimu mkoani Dodoma kuwa ni moja ya sababu ya ufaulu duni. Nyumba hii inadaiwa kuishi walimu katika moja ya mikoa hapa nchini (PICHA YA FIKRA PEVU BLOG)


WADAU wa elimu mkoani hapa wamekutana kujadili changamoto zinazoufanya mkoa kuburuza mkia katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo.


Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge amesema lengo la kikao hicho ni kuhakikisha kinamalizika kwa kuweka mikakati itakayoweza kuukwamua mkoa kielimu.

Ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha wadau hao ambacho kitaibuka na mikakati kabambe itakayochochea ufaulu mzuri kwa wanafunzi wake.

Wadau hao wamekutana baada ya mkoa kugubikwa na aibu ambapo katika kipindi cha miaka mitatu umekuwa miongoni mwa mikoa iliyoburuza mkia kwa kushika nafasi ya 24 kati 26 za mikoa yote ya Tanzania Bara.

Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje amesema nyumba duni wanazoishi walimu wa mkoa huo zinasababisha washindwe kufundisha kwa ari kubwa.

"Walimu wanaishi katika mazingira magumu, kwa hali hii hawawezi kutoa elimu bora, Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kujenga nyumba zao.

Vile vile amezitaka mamlaka zinazohusika kuangalia ikama ya walimu hususan katika maeneo ya vijijini.

Mbunge wa Viti Maalumu, Fatma Taofiq aliitaka Serikali kuweka mikakati ili kuhakikisha wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani yao ya kidato cha pili na kuingia kidato cha tatu, wafanye vizuri pia katika mitihani yao ya kidato cha nne.

Diwani wa kata ya Kikombo, Yona kusaja amesema walimu wapatiwe stahiki zao kwa wakati na kutengenezewa mazingira bora ya kuishi ili wapate morari wa kufanya kazi.


No comments:

Post a Comment