Thursday, 22 February 2018

Wafanyakazi wa nyumbani waandamana kulalamikia mazingira ya kikazi KenyaWAFANYAKAZI wa ndani jijini Nairobi wamejumuika kuandamana wakitoa mwito kwa serikali kuwatambua kama wengine ili na wao waweze kupata manufaa ya ajira kama  bima ya afya, likizo ya uzazi na malipo ya uzeeni.

Mara nyingi, mfanyakazi wa nyumbani anapokuwa mgonjwa, jambo la kwanza mwajiri anachofikiria ni kumfukuza kazi, ukizingatia sheria nchini Kenya, wafanyakazi wa nyumbani wana na haki sawa na mfanyakazi mwingine yeyote.
Wanapokuwa wagonjwa, wafanyakazi wa nyumbani wana haki ya kulipwa siku saba za likizo. Likizo yao ya kila mwaka haipaswi kuwa chini ya siku 21.
Kisheria, waajiri wanatakiwa kuchangia malipo ya bima ya afya na hazina ya malipo ya uzeeni.
Ruth Khakame, mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Wafanyakazi wa nyumbani anasema "wafanyakazi wa nyumbani wamekuwa wakifutwa kazi kwa sababu ya ugonjwa, kila siku tunashugulikia kesi za aina hii"
Kwa mujibu wa shirika la Kituo cha Sheria, wafanyakazi wa nyumbani ni miongoni mwa makundi yanayokumbwa na changamoto zaidi.
Muungano wa wafanyakazi wa nyumbani, ambao umesajili zaidi ya wafanyakazi wa nyumbani 16,000, umekuwa ukiandaa vikao mara kwa mara kusikiliza malalamiko na kuwahamasisha wanachama.
Beatrice Atieno, amefanya kazi hii kwa miaka 15 na huwa anahudhuria vikao hivi "unaweza kupata kuwa unafanyia mtu kazi kwenye nyumba yake na hakuheshimu, hakuamini, ikifika wakati wa chakula anakubagua, anakupatia chakula kidogo, huwezi kushiba, na wewe ndio unamtunza mtoto wake, na wewe ndiye unachunga nyumba yake".
Kwa mujibu wa Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) asilimia 30 ya wafanyakazi wa nyumbani huwa ni watoto. Wanawake wanajumuisha asilimia kubwa.
 Chanzo BBC

No comments:

Post a Comment