Tuesday, 27 February 2018

Wahadhiri wakutana kujadili mustakabali wa elimu


     Waziri wa Elimu Prof. joyce NdalichakoSuleman Kasei

WADAU wa elimu nchini wamepaza sauti kwa Serikali wakiitaka ije na sera ambayo itarejesha heshima ya elimu na walimu ambayo imetoweka kwa sasa.

Aidha, wadau hao wameitaka Serikali kuangalia uwezekano wa kuifanya Wizara ya Elimu kuwa msimamizi mkuu wa sekta ya elimu na wizara nyingine kufuata yanayopitishwa na wizara hiyo.


Wadau hao walipaza sauti hizo jana wakati wakitoa michango yao baada ya uwasilishaji wa ripoti ya mwaka kuhusu usawa katika utoaji wa elimu iliyotolewa na Kitengo cha Uwezo kilichopo ndani ya Shirika la Twaweza.

Akichangia baada ya uwasilishaji wa ripoti hiyo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishiriki Dar es Salaam (DUCE), Dk. Luka Mkonongwa amesema wizara ya elimu inachezewa hali ambayo ni hatari kwa nchi.

Dk. Mkonongwa ameongeza kuwaa wakati wa kutoa elimu katika muktadha wa elimu tu na si elimu bora umepitwa na wakati hivyo jitihada za kuibadilisha sera inayosimamia sekta hiyo zinahitajika.

Amesema hakuna sababu ya kufanyika uamuzi unaogusa elimu bila kushirikisha wataalam wa sekta husika jambo ambalo linaonekana kujitokeza katika elimu.

“Elimu ya nchi hii imezungukwa na vizingiti mbalimbali ambapo ukiangalia sababu kubwa ni kukosekana ushirikishwaji wa wadau wa elimu kama ilivyo sekta nyingine,” amesema.

Amesema kuwa kumekiwepo na mipango mbalimbali itakayoonesha dhamira ya kuipigania elimu lakini kiuhalisia utekelezaaji unakwama kutokana na watekelezaji kutokuwa tayari.

Mkonongwa amesema wakati wa kupigania uwepo wa wizara rasmi ya elimu ni huu ili kuhakikisha sera inayopitishwa inatekelezwa kwa nguvu zote.

Kwa upande wake Dk. Lulu Mahai Mhadhiri Mwandamizi Shule ya Elimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema pamoja na uwepo wa sera nzuri jitihada zinahitajika katika kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi hasa wa shule za serikali.

Dk. Mahai amesema pia serikali inao wajibu wa kuwajengea uelewa wazazi kutambua umuhimu wa elimu hali ambayo itaongeza ufaulu katika shule za serikali na dhana kuwa shule hizo wanafunzi wake wanafeli itaondoka.

Mhadhiri huyo ametoa mwito kwa Serikali kufikiria maslahi ya walimu ili kuchochea matokeo chanya kwani ni dhahiri kuwa maslahi duni ni sababu ya matokeo mabaya.

Mmiliki wa Shule ya Sekondari ya Kifai Modern, Joseph Mbando amesema sera ya elimu iliyopo inawanyima nguvu walimu wakuu hali ambayo inachangia wakati mwingine kufanya kazi katika mazingira magumu.

No comments:

Post a Comment