Wednesday, 21 February 2018

Wakandarasi wazawa malizeni kwa wakati miradi ya ujenzi wa barabara -Profesa MbarawaWaziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na uongozi wa wilaya ya Urambo, alipokutana nao katika ziara yake ya kikazi ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Urambo-Kaliua yenye urefu wa KM 28 inayojengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Tabora.


WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewataka makandarasi wazawa wa kampuni ya Samota, Anam na Jossam JV wanaojenga barabara ya Urambo-Kaliua yenye urefu wa KM 28 kwa kiwango cha lami, kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa muda uliopangwa.

Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo katika kijiji cha Motomoto, wilaya ya Urambo mkoani Tabora alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua mtandao wa barabara mkoani humo ambapo hakuridhishwa na kasi ya ujenzi huo.

“Nataka nione kazi za ujenzi zinafanyika kwa haraka, kwani uzoefu unaonesha baadhi ya makandarasi wazawa wamekuwa na kasi ndogo, hivyo mjipange vizuri ili barabara ikamilike kwa wakati,” amesema.

Ameongeza kuwa nia ya Serikali ni kuwajengea makandarasi wazawa uwezo ili waweze kutekeleza miradi mikubwa mingine ya ujenzi hapa nchini lakini haitasita kuwanyima iwapo wataonesha kuchelewesha miradi hiyo huku wakijenga kwa viwango visivyoridhisha.

“Mkandarasi mzawa atakayechelewesha mradi wowote wa ujenzi hatapewa kazi nyingine kwa sababu atakuwa amechelewesha maendeleo ya wananchi,” amesisitiza Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuwalipa makandarasi wazawa kwa wakati ili waweze kutekeleza miradi yao kwa ufanisi.

Naye Mbunge wa jimbo la Urambo, Magreth Sitta, amemueleza Waziri Prof. Mbarawa kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu kwa wananchi wa wilaya yake na Kaliua na hata mikoa jirani kwani usafirishaji wa mazao na abiria utarahisishwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Angelina Kwingwa amesema wamejipanga vema kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wazawa hao, na kuahidi kuwasimamia ili wamalize kazi hiyo kwa wakati na kwa kiwango stahiki.

Awali akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani humo Mhandisi Damian Ndibalinze, amesema mkandarasi ameshapewa fedha za mradi hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha mradi huo na kuahidi kuwasimamia ili wakamilishe kabla ya mwaka 2020.No comments:

Post a Comment