Friday, 23 February 2018

Wakimbizi watano wa Congo DRC wafariki katika makabiliano na polisi nchini Rwanda

         Magari ya kubeba wagonjwa yalionekana eneo la tukio


POLISI inasema watu 5 wameuawa miongoni mwa wakimbizi wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ambao walikuwa wakitawanywa huku wengine 27 wakijeruhiwa wakiwemo polisi 7 miongoni mwao.
Msemaji wa polisi, Theos Badege amesema polisi ililazimika kutumia nguvu ili kuvunja kile kilichokuwa kimeonekana kama kambi mpya ya wakimbizi kwenye makao ya shirika la umoja wa mataifa la wakimbizi na kwamba walizusha ghasia dhidi ya polisi kwa kurushia mawe, vyuma na chupa.
Tayari wakimbizi 15 wamekamatwa na wanahojiwa na polisi amebainisha Badege.
Taarifa kutoka upande wa wakimbizi zinasema viongozi wao hawajulikani walipo huku ikikisiwa kuwa wengine wamekufa, kutoweka,  kuzuiliwa au kuendelea na matibabu hospitalini.
Wakimbizi hao waliandamana siku 4 zilizopita wakitoka katika kambi yao ya Kiziba hadi Shirika la Umoja wa Mataifa kushinikiza warudishwe nchi mwao au watafutiwe nchi ya tatu.
Kambi ya kiziba inahifadhi wakimbizi wapatao 17,000 waliotoroka Congo miaka 22 iliyopita.
Mmoja ya wakimbizi waliohusika pakubwa kuwasafirisha waathiriwa hospitali ambaye alizungumza na mwandishiu wa BBC Yve Buchana amesema kwanza wamepiga risasi, tukawaambia kwamba hatupambani nao, wakaendelea kupiga risasi watu wakatapakaa kila sehemu, wakaendelea kufyatua risasi na wengine wakaanza kuanguka ,mimi nimeshuhudia watu watatu waliokufa, kuna majeruhi kadhaa tuna wasi wasi kwamba mle ndani kunaweza kuwepo maiti nyingi''
Kulingana na mwandishi huyo alishuhudia magari ya kubeba wagonjwa ama Ambulance yakipishana na magari ya polisi yakiwa yanabeba majeruhi na watu wengine walioonekana kuwa katika hali mahtuti.
Amesema upande wa polisi hakuna tamko lolote lililotolewa kufikia sasa licha ya kamanda wa jeshi kanda ya magharibi kumwambia kwamba wakimbizi wamechokoza polisi na kuwarushia mawe.
Tangu jana eneo hilo lilikuwa limezingirwa na vikosi vya polisi waliojihami sawa wakionekana kuwa tayari kwa lolote. Serikali iliiwashutumu wakimbizi kwa kufanya mgomo na kukiuka sheria za nchi na kusema itaanzisha upelelezi kuhusu chanzo cha mgomo huo na kuwaadhibu wahusika.
Wakimbizi wenyewe walisema waliamua kukita kambi kwenye ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (NHCR), wakilalamika kuchoka na maisha wanayotaja kuwa mabaya nchini Rwanda huku wakishinikiza kurudishwa nchini mwao au katika nchi nyengine ya tatu.

No comments:

Post a Comment