Thursday, 15 February 2018

Wanafunzi wa vyuo watakiwa kujitoa kufundisha wenzaoWanafunzi kama hawa wanapojifunza masomo yote yakiwemo ya sayansi, taifa linajitoshereza kwa wataalamu wake.
Joyce Kasiki
WANAFUNZI walimu wa masomo ya Sayansi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, wameombwa kutumia muda wao wa ziada kujitolea kufundisha katika shule za mkoani hapa ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu wa masomo hayo.

Akizungumza na wanahabari mbele ya Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Peter Msoffe, mwanafunzi wa mwaka wa tatu kutoka Chuko Kikuu Kishiriki cha Dar es Salam (DUCE), Emijidius Cornel ambaye ni mwanzilishi wa kampeni ya wanafunzi hao kujitolea alisema wao kama wasomi wanapaswa kutumia muda wao mwingi kujitolea kufundisha badala ya kuchati kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo Whatsap.

Cornel amesema,hatua ya wanafunzi hao kujitolea ni dhahiri kuwa inaweza kuongeza ufaulu kwa mkoa wa Dodoma kwani wataziba pengo la upungufu wa walimu hususan wa masomo ya sayansi katika baadhi ya shule za mkoa huu.

“Mimi ndiye mwanzilishi wa kujitolea na nimehamasisha wanafunzi pale DUCE wamepatikana 400 na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanafunzi 100, na tayari uzinduzi tumeshafanya,

“Sasa nikaona kampeni hii niifanye pia katika chuo cha UDOM lakini lengo ni kuvifikia vyuo vikuu vyote nchini ili wanafunzi wa masomo ya sayansi wajitolee kufundisha katika maeneo yao,”amesema Cornel.

Rais wa Serikali ya wanafunzi wa UDOM, Francisco Nzalalila amesema amelipokea wazo hilo na atafanya utaratibu wa kuzungumza na wanafunzi wa masomo hayo chuoni hapo ili waanze mpango huo.

“Ingawa mwanzoni nilipata kigugumizi kutokana na muda wa wanafunzi hao ambao wanapaswa kujisomea ili wafanye vizuri katika mitihani yao, lakini baadaye pia nikaona ni fursa kwao katika kujenga uzoefu, lakini pia wanatengeneza ‘net work’ ambayo itawasaidia watakapohitimu masomo yao chuoni,” amesema Nzalalila.

Amesema wao kama wanafunzi wasomi wanatamani kuwa sehemu ya kutatua changamoto za kielimu kwani kwa hatua waliyofikia, uwezo wa kufanya hivyo wanao kwa muda ambao wanakuwa hawana vipindi chuoni.

Kwa upande wake Profesa Msoffe amesema, wazo hilo ni zuri kwani litawapa wanafunzi uzoefu wa kufundisha darasani lakini pia watarudisha suala la uzalendo.

“Wazo hili ni zuri, linarudisha uzalendo ambao ulikuwepo zamani, maana zamani watu walikua wanafanya uzalendo kwa kutumia walivyo navyo kwa ajili ya taifa, lakini siku hizi hakuna kabisa uzalendo,”amesema Profesa Msoffe

Hata hivyo, ametoa tahadhari kuwa pamoja na kuwa ni mpango  mzuri wanapaswa kuangalia suala la muda ili wanafunzi wasije kukazingatia zaidi vipindi wanavyofundisha badala ya kujikita kwenye masomo yao pia mpango huo usiwe na vitu vingine nyuma ya pazia maana hautafika mbali.

No comments:

Post a Comment