Saturday, 24 February 2018

Watiwa mbaroni kwa kukutwa wakitaka kuuza pembe za ndovu

                           Kamanda wa Polisi Mkoa Dodoma, Gilles Muroto               

Mwandishi Wetu, Dodoma

WATU wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma baada ya kukamatwa wakiwa katika harakati za kutaka kuuza vipande vya pembe za ndovu.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, akizungumza na wanahabari ofisini kwake, amesema washukiwa hao walikutwa na vipande hivyo vyenye uzito wa kilo 2.450, sawa na thamani ya sh. milioni 67.5.

Aliwataja washukiwa hao kutoka maeneo tofauti ya wilaya ya Chemba mkoani hapa, kuwa ni Juma Gindae (50), mkulima na mkazi wa Kwamatoro , Patrick Mwaluko (49), mkulima wa Kidoka, Daudi Masinga(22), dereva bodaboada wa Kidoka, na Halifa Saluti (21), Dereva bodaboda pia mkazi wa wilaya hiyo.

Amesema, tukio hilo limetokea Februari  20 mwaka huu, wilayani Kondoa, mkoani Dodoma ambapo washukiwa hao walikuwa katika harakati za kufanya mauziano  katika eneo la Benki ya NMN Kondoa.

Kamanda Muroto amesema, baada  ya  polisi kupata taarifa za tukio hilo walikwenda eneo hilo ambapo waliwakuta na kuwazingira katika eneo hilo la Benki wakati wanasubiri fedha kutoka kwa mnunuzi wa vipande hivyo.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya washukiwa kuona wamezingirwa na polisi walijaribu kutoroka kwa kuwatishia askari kwa visu lakini waliwafyatulia risasi sita hewani na kufanikiwa kuwakamata wote.

Amesema washukiwa hao pia walikamatwa wakiwa na pikipiki mbili zenye namba MC 670 BEF na MC 828 AXJ zote aina ya Fekon rangi nyekundu.

Katika tukio jingine jeshi hilo limekamata watu watatu kwa kosa la kumiliki silaha kinyume cha sheria. Tukio hilo lilifanyikaFebruari 18 katika kijiji cha Ilangali, tarafa ya Mpwayungu, wilayani Chamwino.

Watuhumiwa hao ni Kachinga Labani (38), mkulima mkazi wa Ilanagali, Shack Chale (31), mkulima na mkazi wa Ilangali, Samweli Alfa (37), mkulima na mkazi wa Ilangali ambao wote wanamiliki siraha aina ya gobore kinyume cha sheria.

Amesema,silaha hizo walikuwa wakizitumika katika uwindaji haramu katika hifadhi ya Ruaha iliyopo jirani na kijiji hicho na uhalifu mbalimbali katika vijiji vya jirani ambapo siraha tatu zote zimekatwa”amesema Muroto.No comments:

Post a Comment