Thursday, 22 February 2018

Wazazi wa wanafunzi watoro Chamwino kukiona

                                              Vumilia Nyamoga 


MKUU wa wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga amesema miongoni mwa mikakati iliyojiwekea wilaya yake ili kuinua kiwango cha ufaulu ni mahakama inayotembea ambayo itawahukumu wazazi wa wanafunzi watoro.

Akitoa taarifa kuhusu kuinua kiwango cha ufaulu  wilaya mwake mbele ya Mkuu wa mkoa wa  Dodoma, Dk. Binilith Mahenge,  Nyamoga amesema mahakama hiyo itasaidia kutoa hukumu ya haraka kwa wazazi wanaowakumbatia watoto wao watoro wa shule.

"Katika wilaya yetu lipo tatizo la utoro shuleni ambalo kwa namna moja ama nyingine, linachangia kushusha kiwango cha ufaulu kwa wilaya na mkoa kwa ujumla.

"Hivyo, mikakati tuliyojiwekea ni pamoja na kuwa na mahakama inayotembea ambayo itawahukumu kwanza wanafunzi watoro shuleni, lakini pia wazazi wanaoishi na wanafunzi hao wanaoacha kwenda shule kwa sababu zozote zile," amesema Nyamoga.

Ameongeza kuwa ni dhahiri mahakama hiyo itafanya uamuzi na kutoa hukumu kwa haraka zaidi bila watuhumiwa kupoteza ushahidi kuliko ilivyo sasa.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu we wilaya ya Dodoma, Deogratius Ndejembi amesema mikakati iliyojiwekea wilaya hiyo ni pamoja na kuwa na usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa masuala ya elimu wilayani humo.

Kwa upande wake, Dk. Mahenge amewataka viongozi wote wa wilaya za mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanasimamia vema mikakati waliyoiweka na kuitekeleza na siyo kwenda kuifungia kwenye kabati.

Katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia 2015-2017 ,mkoa wa Dodoma umeshika nafasi ya 24 katika mitihani ya kidato cha nne kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara. 

No comments:

Post a Comment