Wednesday, 28 March 2018

Abiy Ahmed ateuliwa kuwa waziri mkuu Ethiopia


Dk. Abiy Ahmed

DAKTARI Abiy Ahmed, anayetoka jamii ya Oromo yenye watu wengi Ethiopia, amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa muungano unaotawala EPRDF,  hatua itakayomfanya kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo.
Ahmed alichaguliwa kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali na atachukua wadhifa huo kutoka kwa Hailemariam Desalegn aliyetangaza ghafla kujiuzulu mwezi uliopita.
Taifa hilo kwa sasa liko katika hali ya dharura iliyotangazwa kwa ajili ya kumaliza maandamano ya takriban miaka mitatu dhidi ya serikali.
Dk. Ahmed, 42, ametazamwa na wengi kama mwenye kuzungumza kwa uwazi, mwenye ujuzi na uzoefu na mwenye kukumbatia uongozi wa kuwashirikisha wote. Anaaminika kuwa na ufuasi mkubwa miongoni mwa vijana wa Kioromo na pia katika jamii nyingine.
Wakosoaji wake hata hivyo wanasema ni mtu wa ndani katika chama na hivyo basi, hakuna matumaini kwamba matakwa ambayo yamekuwa yakiitishwa na waandamanaji.
2015
Dk. Ahmed amechaliwa baada ya mkutano wa siku kadhaa wa viongozi wa muungano tawala wa Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF). Ahmed anatoka katika kabila kubwa zaidi nchini Ethiopia la Oromo ambalo limekuwa likifanya maandamano ya kuipinga serikali tangu mwaka 2015.
Majuzi alichaguliwa mwenyekiti wa chama cha Oromo People's Democratic Organisation (OPDO). Miaka ya nyuma aliwahi kuhudumu kama waziri na alikuwa na mchango mkubwa katika kuanzisha shirika la ujasusi la taifa hilo.
Wakosoaji wake hata hivyo wameelezea hofu zao juu ya ikiwa atapewa nafasi na mamlaka ya kutekeleza mageuzi yaliyodaiwa na waandamanaji.
Maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi wamekuwa wakikamatwa na kufungwa tangu maandamano yalipoanza yapata miaka mitatu iliyopita.
Dkt Abiy Ahmed ni nani?
Abiy alizaliwa Agaro Kusini Ethiopia katika eneo la Jima Agosti 15, 1976 na baba Mwislamu kutoka jamii ya Oromo na mama Mkristo kutoka jamii ya Amhara.
Dk. Abiy anaangaliwa kama mwanasiasa mwenye kukubalika ambaye ana siasa ya kuwashirikisha watu katika masuala yanayowahusu na mwenye mafanikio makubwa upande wa elimu na jeshi.
Ana taaluma ya udaktari katika masuala ya amani na usalama kutoka chuo kikuu cha Addis Ababa na ana shahada ya uzamili ya mabadiliko ya uongozi kutoka Chuo Kikuu cha Greenwich, London Uingereza.
Ana shahada ya uzamifu katika usimamizi (MBA) chuo kikuu cha Ashland Leadstar aliyoipata 2013 baada ya kukamilisha masomo yake ya shahada ya kwanza ya Kompyuta kutoka chuo cha habari cha Microlin mjini Addis Ababa mwaka 2001.
Abiy anazungumza vizuri lugha za Afan Oromo, Amharic na Tigrinya, pamoja na Kiingereza. Akiwa kijana mdogo miaka ya 1990, alijiunga na mapambano ya kijeshi dhidi ya utawala wa zamani wa Dergue.
Baada ya kuanguka kwa utawala wa Dergue, alipata mafunzo rasmi ya kijeshi katika chuo cha Brigade Asefa Magharibi mwa Welega na akapanda cheo haraka na kuwa Luteni kanali na baadaye alihudumu kwa kiasi kikubwa katika huduma za ujasusi na mawasiliano.
Mwaka 1995, alihudumu katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Rwanda.
Wakati wa mzozo wa mpaka baina ya nchi yake na Eritrea kati ya mwaka 1998 hadi 2000, aliongoza kikosi cha ujasusi kilichokuwa na jukumu la uchunguzi katika eneo lililochukuliwa na vikosi vya jeshi la Eritrea.
Mwaka 2007, alianzisha shirika la Ethiopia la Mtandao wa Taarifa za Usalama (INSA) ambapo alihudumu kama mjumbe wa bodi ya Mawasiliano ya simu ya Ethiopia, Ethiopia Televisheni na mashirika mengine ya serikali.
Mwaka 2010, aliondoka katika shirika la INSA na kujiunga na siasa kama mjumbe wa kawaida wa OPDO kabla ya kujiunga katika kamati tendaji ya chama hicho mwaka 2015.
Baadaye mwaka huo, alichaguliwa kama mbunge wa eneo la Agaro anakotoka.Wakati wa muhula wake bungeni yalishuhudiwa makabiliano baina ya Waislamu na Wakristo kwenye jimbo lake.
Makabiliano hayo yalimfanya abuni mkakati wa kudumu wa tatizo hilo, kwa kubuni jukwaa lililojulikana kama "jukwaa la kidini kwa ajili ya amani ".
Mnamo mwaka 2016, alihudumu kwa muda mfupi kama waziri wa sayansi na teknolojia. Aliacha wadhfa wake wa uwaziri kuongoza halmashauri ya chama cha OPDO hadi alipopanda cheo na kupata uenyekiti wa chama hicho.

No comments:

Post a Comment