Wednesday, 14 March 2018

Angela Merkel kuingoza Ujerumani muhula wa nne


SIKU 171 baada ya uchaguzi mkuu, bunge la Ujerumani Bundwestag limepiga kura hii leo kumchagua Angela Merkel kuwa kansela kwa muhula wa nne mfululizo.

Mchakato wa kumchagua kansela umeshakamilika katika bunge la shirikisho Bundestag. Lakini kama ilivyokuwa miaka minne iliyopita, safari hii pia Angela Merkel hakupata kura zote za wabunge wa vyama vinavyounda serikali ya muungano.

Wabunge 364, kati ya 399 wa vyama hivyo ndio waliomuunga mkono mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 63, ikimaanisha 35 kati ya wabunge wa kambi yake hawakumuunga mkono.

Wabunge 315 wamempinga na tisa wamejizuia kupiga kura.  Wabunge 702 kati ya 709 wa shirikisho ndio waliohudhuria kikao cha leo na kura za wabunge 692 zimehesabiwa kuwa halali.

Baada ya kuchaguliwa Angela Merkel alimjibu spika wa bunge Wolfgang Schauble na kusema anayakubali matokeo ya uchaguzi.

Baada ya kuchaguliwa kwa wingi wa vyama tawala, Angela Merkel ameelekea katika kasri la rais ambako rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier alimkabidhi hati ya kuchaguliwa kwake kabla ya kurejea tena bungeni kuidhinishwa na spika wa bunge hilo Wolfgang Schäuble.

Mwanzoni mwa muhula wake wa tatu, miaka minne iliyopita, Angela Merkel alipungukiwa na kura 42 kutoka wabunge wa vyama tawala vya CDU/CSU na SPD. Na hata mihula miwili ya awali, mwaka 2005 na 2009 sio wabunge wote wa vyama tawala waliomuunga mkono.

Naibu mwenyekiti wa chama cha upinzani cha FDP Wolfgang Kubicki amesema matokeo ya uchaguzi wa kansela yanaashiria muungano sio wa vyama vikuu, bali  ni wa vyama vidogo. Anaashiria kuna wabunge wa SPD sawa na wa CDU ambao hawakumuunga mkono kansela.

Amesema uamuzi wao hauashirii mema kwa serikali ya muungano.
Kwakua zoezi la uchaguzi katika bunge la shirikisho ni la siri, hakuna anaeweza kusema kwa uhakika wangapi miongoni mwa wabunge wa vyama tawala hawakumpigia kura au wangapi kutoka vyama vya upinzani wamempigia kura Angela Merkel.

Kama ilivyotajwa katika sheria msingi ya Ujerumani, magari ya fakhari yatakuwa yakienda na kurudi kati ya bunge la Reichtag na Schloss Bellevue , umbali wa kilomita mbili, kupokea hati za kuchaguliwa kwao, tangu kansela mpaka mawaziri wa serikali yake na kurejea baadaye bungeni kuidhinishwa.
Kikao cha kwanza cha baraza jipya la mawaziri kinaitishwa jioni hii.

No comments:

Post a Comment