Dk. Faustine Ndugulile
Ismail Ramadhani
SERIKALI imesema ugonjwa wa shinikizo la macho
‘Glaucoma’, huathiri zaidi watu wenye umri wa miaka 40 na Tanzania na inakadiriwa
kuwa na asilimia 4.2 sawa na watu 440,000 wanaougua tatizo hilo.
Naibu Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile amesema
hayo Dar es Salaam wakati akizungumzia wiki ya maadhimisho ya utoaji wa elimu
kuhusu ugonjwa huo.
Maadhimisho
hayo yalianza Machi 11 na yataendelea hadi Machi 17, mwaka huu. Aidha, amesema
kwa bahati mbaya asilimia 70 hadi 90 ya watu wenye ugonjwa huo, hawajijui.
Glaucoma ndiyo
chanzo kinachoongoza kwa idadi ya watu wasioona. Amesema Tanzania inakadiriwa
kuwa na watu milioni 1.7 wenye matatizo ya kutokuona vizuri, kunakosababishwa
na matatizo mbalimbali ikiwemo kuwa na mtoto wa jicho, upeo mdogo wa macho
kuona na shinikizo la macho linalojulikana kitaalamu kama ‘Glaucoma.
Amesema katika
mwaka 2017, watu 13,240 tu waliohudhuria kwenye vituo vya tiba wakiwa na tatizo
la shinikizo la macho, idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na watu walio katika
hatari ya kuwa na ugonjwa huo ambao wapo katika jamii na hawajagunduliwa.
“Ugonja huu wa
shinikizo la macho ni moja kati ya kundi la magonjwa ya macho yanayoshambulia
mshipa wa fahamu unaopeleka mawasiliano ya uoni kwenye ubongo yaani neva optiki
ili kuweza kutafsiri kile kinachoonekana,” amesema Ndugulile.
Ameongeza kuwa
ugonjwa huo, husababisha upofu kwa taratibu sana kwa siku hadi siku bila dalili
yoyote katika hatua ya awali, na ili kuweza kugundua iwapo mtu ana ugonjwa huo,
upo umuhimu wa kupima macho japo mara moja kwa mwaka, hasa kwa makundi yaliyo
hatarini kama mtu haoni tatizo lolote kwenye macho.
“Ugonjwa huu
hauna dalili zozote wakati wa hatua za awali na ndiyo maana wakati mwingine
huitwa mwizi wa kimyakimya wa uwezo wa macho kuona, kwa kuwa huleta ulemavu wa
kutokuona katika umri mdogo na taifa kupoteza nguvu kazi,” amesema.
Kuhusu
maadhimisho hayo amesema kutakuwepo na shughuli za elimu ya afya ya macho
pamoja na upimaji wa afya ya macho kwenye hospitali mbalimbali nchini na katika
kliniki zote za macho na elimu pia itatolewa kuhusu ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment