Wednesday, 21 March 2018

Australia Tanzania Society yaipiga jeki Muhimbili


Mkurugenzi wa Australia Tanzania Society, James Chialo (kushoto), akimkabidhi Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Muhimbili, Dk. Julieth Magandi vitanda 14. Katikati ni Mkuu wa Idara ya Uuguzi na Mazingira Muhimbili, Zuhura Mawona.

Jumanne Juma

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), jana imepokea msaada wa vitanda 14, magodoro 12 pamoja na drip stands kutoka Australia Tanzania Society ambavyo vitasaida kuimarisha utoaji wa huduma hospitalini hapo.

Akipokea msada huo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dk.  Juliethi Magandi amesema kwa muda mrefu hospitali imekua na ushirikiano na tasisi hiyo katika masuala mbalimbali ikiwemo kufanya  upasuaji wa ubingwa wa juu.

“Kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru rafiki zetu hawa Australia Tanzania Society kwa msaada huu walioutoa kwani tumekua tukishirikiana kwa zaidi ya miaka mitatu sasa,” amesema Dk. Magandi.

Amefafanua kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ina vitanda 1,507 na kwamba wajawazito na watoto pekee wanatumia karibu nusu ya vitanda hivyo.  

"Hivyo  msaada huo umekuja wakati muafaka  kwani hospitali bado ina mahitaji kutokana na kutoa huduma zake kila siku kwa saa 24.

 “Kati ya vitanda hivi 14 tulivyopewa leo (jana), sita tumevileta wodi 35  kwa ajili ya kinamama na vingine 8 tumepeleka ICU namba moja na ICU namba mbili,’’ amefafanua Dk. Magandi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Australia Tanzania Society, James Chialo amesema msaada huo umegharimu zaidi ya sh. milioni 25 na kwamba lengo ni kuboresha huduma za afya hususanikatika hospitali za umma.

“Kutoa ni moyo si utajiri tutaendelea kushirikiana katika kuboresha huduma za afya kadiri hali inavyoruhusu  nitoe mwito kwa wadau wengine kuendelea kushirikiana ili tuboreshe huduma za afya nchini,”amesema Chialo.

No comments:

Post a Comment