Thursday, 1 March 2018

Bilioni 3 za Tasaf zanufaisha wananchi Namtumbo


 Wanufaika wa Tasaf wilaya ya Namtumbo ambao wamejiunga katika vikundi vya ujasiriamali

Yeremias Ngerangera

HALMASHAURI ya  wilaya ya Namtumbo,  mkoani Ruvuma imetumia zaidi ya sh. bilioni 3.6 kwa  wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf),  tangu  mpango huo ulipoanzishwa  mwaka 2015.

Mratibu wa Tasaf wilaya Namtumbo, Raphael  Mponda amesema tangu mpango  huo uanzishwe  na serikali, halmashauri hiyo imewalipa wanufaika wake kwa  awamu  16 .


Aidha, Mponda amebainisha mafanikio  ya mpango  huo kwa wanufaika  wa kaya  maskini kuwa ni pamoja  na kaya 2073 kati ya kaya 5559 zimejiunga na mfuko wa  afya  ya  jamii (CHF).

Mahudhurio ya watoto  shuleni yameongezeka, kaya zinazonufaika zimeboresha makazi yao na  watoto 181 wa  kaya  maskini waliohitimu darasa la saba mwaka 2017, wamejiunga na kidato cha kwanza mwaka huu (2018).

Wanufaika wa mpango huo, Zena Faraji  wa kijiji  cha Suluti  na Ridhiki  Gehu wa Nahoro wamesema mpango wa kunusuru kaya maskini umeboresha maisha yao kwa kuwa wameweza kujikita katika kilimo na kufuga mifugo kutokana na fedha hizo.

Pia wanufaika hao wamesema wamejiunga katika vikundi vya kaya maskini vya kuweka na kukopa ambavyo  vinawawezesha kuweka fedha na kukopa kwa ajili ya kufanya biashara ndogondogo.

Kaimu  ofisa  maendeleo ya jamii, Owigo Phinias pamoja na mambo mengine amesema halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ina vikundi 28 vya  wanufaika wa kaya maskini ambapo baadhi vimefika  hatua ya kupata  usajili baada ya kutimiza  masharti  na vingine vinaendelea  na usajili ili kuwawezesha kukopa fedha katika mfuko wa wanawake  unaotolewa  na halmashauri hiyo.

Mmoja wa wanufaika wa Tasafu wilaya ya Namtumbo akieleza mafanikio aliyapata kutokana na fedha za mpango huo.

Halmashauri  ya wilaya  ya Namtumbo ina  kaya  5559  zinazonufaika na mpango wa serikali wa kunusuru  kaya  maskini  katika  vijiji  42 kati ya 61 vya halmashauri  hiyo.

No comments:

Post a Comment