Sunday, 18 March 2018

Bobali kusimamia hoja nne bungeniHamidu Bobali  

Suleiman Kasei

MBUNGE wa Mchinga mkoani Lindi, Hamidu Bobali amesema atatumia mkutano wa 11 wa Bunge la 11 kuwasilisha hoja nne ikiwemo ya kuitaka Serikali kutoa ruzuku kwa vijana wa vijijini wanaotaka kuanzisha mashamba ya kilimo cha korosho.

Bobali ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wandishi wetu jijini Dar es Salaam ambapo aliweka bayana kuwa kundi kubwa la vijana vijijini limesahaulika pamoja na ukweli kuwa linadhamira ya kujikwamua kiuchumi.

‘Katika Bunge lijalo ambalo linatarajiwa kuanza Aprili 3 mwaka huu nitakuwa na hoja kubwa nne ambazo zinagusa jamii ninayoiongoza ni imani yangu kuwa ufumbuzi ukipatikana katika eneo hilo mabadiliko ya kiuchumi yataonekana,” amesema.

Ameongeza kuwa katika jimbo lake na mkoa mzima wa Lindi ipo ardhi ya kutosha na inayostawi mazao mbalimbali ya biashara na chakula kama vile ufuta na korosho hivyo ana amini kukiwepo mkazo wa kutosha vijana watainuka kimaendeleo.

“Nakwenda kutoa hoja za kuitaka serikali itoe ruzuku kwa vijana walipo vijijini wale wanaotaka kuanzisha mashamba ya mikorosho iwapatie mikopo nafuu ili baada ya miaka mitatu serikali iwe inapata mapato makubwa ya ushuru lakini pia tutakuwa tumewasaidia kupata ajira ya kudumu,” amesema.

Bobali amefafanua kuwa jambo la pili ambalo atalisimamia katika Bunge la Bajeti ni kuitaka serikali itoe chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari na kwamba huduma hiyo ichangiwe kati ya serikali na wazazi.

Amesema kitendo cha kuwakataza wazazi wasitoe michango ya chakula shuleni ni kutaka kushusha kiwango cha ufaulu kwa watoto wanaosoma shule za serikali hasa vijiji ambapo walimu ni wachache.

Mbunge huyo amesema changamoto nyingne inayowakabiliwa wapiga kura wake ni uhaba wa maji hivyo atahakikisha serikali inaacha porojo na takwimu zisizo na uhalisia badala yake mfuko wa maji utumike kikamilifu kuondoa tatizo la maji nchini hususan vijijini.

“Huduma ya maji ielekezwe ipasavyo vijijini ili kukamilisha kwa vitendo kauli mbiu ya kumtua ndoo mama kichwani kwani imekuwa ikisemwa bila vitendo,” amebainisha.

Aidha, Bobali amesema atatumia mkutano huo kumtaka waziri husika na Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura), kuachana na utaratibu wa manunuzi ambao unachukua muda mrefu hadi kufikia miezi sita ili mchakato kukamilika huku miundombinu ya barabara ikiendelea kuharibika.

Bobali atanabaisha kuwa amejitolea kuwapigania wananchi wa Mchinga hivyo hatanyamaza pale ambapo anaona kuna mambo hayaendi sawa hasa katika kuwainua kiuchumi.

No comments:

Post a Comment