Wednesday, 28 March 2018

China, Korea Kaskazini zathibitisha Kim Jong-un aliyezuru China


Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un (wa pili kulia) akiwa na mwenyeji wake Xi Jinping pamoja na wake zao.


CHINA na Korea Kaskazini zimethibitisha kuwa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un amezuru China.

Uthibitisho huo umekuja baada ya kuwepo tetesi kuwa ofisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Korea Kaskazini amefanya ziara ya ghafla China kuwa huenda alikuwa ni kiongozi huyo (Kim Jong-un).
Ziara hiyo, ndiyo ya kwanza inayofahamika ya Kim nje ya taifa lake tangu alipochukua mamlaka mwaka 2011.
Kim amefanya "mazungumzo ya kufana" na kiongozi wa China Xi Jinping mjini Beijing, shirika la habari la China, Xinhua limeripoti.
China ni mshirika mkuu wa Korea Kaskazini kiuchumi na baadhi ya wachambuzi wanasema uwezekano wa wawili hao kukutana kabla ya mkutano mkuu wa Kim na viongozi wa Korea Kusini na Marekani ulitarajiwa.
Kim amepangiwa kukutana na Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in mwezi Aprili na Rais wa Marekani Donald Trump hapo Mei.
Ziara hiyo ya Beijing inatazamwa na wengi kama hatua muhimu katika maandalizi ya Korea Kaskazini kuhusu mazungumzo hayo.
Wakati wa ziara hiyo, Kim alimhakikishia mwenzake wa China kwamba amejitolea kuacha kustawisha silaha za nyuklia, kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua. Hata hivyo, amesema atafanya hivyo bila masharti.
"Suala la kumalizwa kwa silaha za nyuklia katika Ras ya Korea linaweza kutatuliwa, lakini iwapo tu Korea Kusini na Marekani watajibu juhudi zetu kwa nia njema, kuunda mazingira ya amani na uthabiti na pia kwa kuchukua hatua za kusonga mbele kwa pamoja kutoka kwa wadau wote kuhakikisha amani inapatikana,” Kim alinukuliwa akisema.
Shirika la habari la Korea Kaskazini, KCNA, lilieleza ziara hiyo kama yenye umuhimu mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na China.
"Ina maana kwa Korea Kaskazini kufafanua msimamo wake na kushirikiana na China, mshirika wake muhimu zaidi," msomi katika Pacific Forum CSIS Andray Abrahamian ameambia BBC.
"Uhusiano huo umekuwa ukidhoofika katika miaka mitano iliyopita na China imekuwa ikitengwa kidiplomasia katika miezi kadha iliyopita. Kutoka kwa mtazamo wa Beijing, hii ni ziara ambayo ilifaa kufanyika kitambo sana," amesema.
Kwa sehemu kubwa, hii ni ziara yenye maana kubwa kwa urafiki wa Korea Kaskazini na China, na ni ishara ya heshima pia, Fyodor Tertitskiy wa shirika la habari la NK News linaloangazia sana taarifa kuhusu Korea Kaskazini amesema.         
"Wana mikutano miwili mikubwa kati ya kiongozi wao na mataifa mengine - mmoja na Seoul na mwingine na Washington - na pengine wanataka kuusikia msimamo wa China pia. KCNA wamesema Xi pia amekubali mwaliko wa kuzuru Korea Kaskazini.
Kim aliwasili akiandamana na mkewe, Ri Sol Ju, Jumapili na wawili hao waliondoka Beijing Jumanne alasiri, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari.
Ziara hiyo ni ya karibuni kwenye msururu wa shughuli nyingi za kidiplomasia tangu Korea Kaskazini na Kusini zilipoanza kuimarisha uhusiano wao wakati wa Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi iliyoandaliwa Korea Kusini.
China iliwasiliana na utawala wa Trump na kuwafahamisha yaliyotokea katika mkutano huo jana Jumanne, serikali ya Trump ilithibitisha.
"Tunatazama hili kama ishara nyingine kwamba kampeni yetu ya kuweka shinikizo kali ndiyo inayozaa matunda na kufanikisha mazingira mwafaka ya mazungumzo na Korea Kaskazini," msemaji wa ikulu ya White House Sarah Huckabee Sanders amesema.
Mwezi uliopita, Trump alichukua hatua isiyo ya kawaida na kukubali mwaliko wa kukutana na Kim baada ya miezi mingi ya uhasama na majibizano pamoja na Korea Kaskazini kufanyia majaribio ya makombora.
Mkutano huo wa Kim na Trump ukifanyika, basi Trump atakuwa rais wa kwanza kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini akiwa bado uongozini.
Chanzo: BBC

No comments:

Post a Comment