Saturday, 31 March 2018

CUF Mwanza yampiga ‘stop’ Maalim Seif


Maalim Seif Sharif Hamad 

Mwandishi Wetu, Mwanza

CHAMA cha Wananchi (CUF) mkoani Mwanza kimempiga marufuku Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kutofanya mikutano na vikao vya kisiasa katika wilaya za Nyamagana na Ilemela zilizoko jijini hapa.

Hatua ya kumpiga marufuku Maalim Seif aliyesimamishwa uongozi na Baraza Kuu la Uongozi la CUF Taifa, imetolewa katika tamko la pamoja la viongozi katika wilaya za Ilemela za Nyamagana mkoani Mwanza.

Viongozi hao waliongozwa na Mwenyeviti wa CUF wa Wilaya ya Nyamagana, Salum Mkumbukwa aliyekuwa ameambatana na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa, Martha Haule na Zainabu Ally.

Wamedai kuwa wamesikia kuwa Maalim Seif anawasili jijini Mwanza kwa siri kupitia mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ili kuhudhuria kongamano la chama cha siasa linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni katika wilaya hizo.

Viongozi hao wamesema wamemwandikia barua kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mwanza, mkuu wa mkoa wa Mwanza na wakuu wa wilaya za Nyamagana na Ilemela kupinga ujio wake.

No comments:

Post a Comment